Na Asha Mwakyonde, DODOMA
WAKALA wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), umeadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake kwa kueleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika utoaji wa huduma za ufundi, usimamizi wa mitambo na maboresho ya miundombinu ya umeme, huku ukiahidi kuendelea kuimarisha ufanisi na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya Taifa.
Akizungumza katika hafla ya maadhimisho ya miaka 20 ya TEMESA iliyofanyika jijini Dodoma Juni 23, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa TEMESA, Kheri Mahimbali, amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi za wafanyakazi, ushirikiano mzuri na Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Amesema katika kipindi hicho, TEMESA imeendelea kupanua wigo wa huduma zake kwa kushirikiana na sekta binafsi, hususan katika matengenezo ya magari, mitambo na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kiufundi inayolenga kuboresha huduma kwa wananchi.
Mahimbali amesema taasisi hiyo imefanikiwa kuboresha miundombinu ya umeme katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo uwekaji na matengenezo ya taa za barabarani, hatua iliyochangia kuimarisha usalama na kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi katika maeneo ya mijini na vijijini.

“Tunaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali na wadau wengine ili kuhakikisha huduma tunazozitoa zinakuwa bora zaidi, zenye ufanisi na tija kwa taifa,” amesema Mahimbali.
Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuzielekeza taasisi za umma kufanya kazi kwa ufanisi, kuongeza tija na kujiendesha kwa misingi ya uwajibikaji ili kuchochea maendeleo ya uchumi wa nchi.
Kwa mujibu wa Mahimbali, TEMESA imejipanga kuimarisha zaidi shughuli zake za kibiashara ili kuongeza mapato yatakayowezesha kuboresha mazingira ya kazi, kuongeza ufanisi wa huduma na kuimarisha maslahi ya watumishi wake.

Aidha, amewapongeza wafanyakazi wa TEMESA kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha majukumu ya taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka 20, akisisitiza kuwa uongozi utaendelea kuboresha ustawi wao ili kuongeza ari na tija kazini.
Mkurugenzi huyo aliwapongeza watumishi wote wa TEMESA kwa kazi kubwa wanayoifanya kila siku huku akieleza kuwa Uongozi utaendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi hao ili kuongeza motisha ya kazi na kuhakikisha wakala huo unaendelea kuwa taasisi bora, yenye ushindani na inayotoa huduma zenye viwango vya juu.


