TANZANIA, UJERUMANI WASAINI MKATABA WA BILIONI 60.7 KUBORESHA HUDUMA YA MAJI MKOANI SONGWE

Na Benny Mwaipaja, Dodoma

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini mkataba wa msaada wa Euro milioni 20 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 60.7 kutoka Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) kwa ajili ya kufadhili mradi wa Uboreshaji wa Huduma za Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira katika miji ya Tunduma na Vwawa-Mlowo, mkoani Songwe.

Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo imefanyika katika Ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba kwa upande wa Serikali ya Tanzania na Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) nchini Tanzania, Bi. Vanessa Eidt.

‎Akizungumza baada ya utiaji saini wa mkataba huo, Dkt. Mwamba alisema kuwa Mradi unalenga kuchangia katika uboreshaji endelevu wa upatikanaji wa maji safi na usafi wa mazingira, pamoja na usimamizi wa rasilimali za maji kwa watu wanaoishi katika miji ya Tunduma na Vwawa-Mlowo.

‎Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (Kulia) na Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) nchini Tanzania, Bi. Vanessa Eidt, wakionesha hati za Mkataba wa msaada wa Euro milioni 20 (sawa na shilingi za Tanzania bilioni 60.7) kwa ajili ya kufadhili mradi wa Uboreshaji wa Huduma za Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira katika miji ya Tunduma na Vwawa-Mlowo, mkoani Songwe, halfa iliofanyika katika Ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.

“Mradi huu utachangia katika kuongeza upatikanaji wa maji salama na safi ya kunywa na huduma endelevu za usafi wa mazingira kwa kujenga miundombinu ya usambazaji maji, kuunganisha wateja, Mtambo wa kutibu majitaka, ununuzi wa magari ya majitaka (exhauster), na ujenzi wa miundombinu ya usafi kwenye taasisi za umma kama vile ujenzi wa vyoo katika shule zilizochaguliwa.”, aliongeza Dkt. Mwamba.

Aidha, Dkt. Mwamba aliishukuru Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani kwa msaada huo muhimu na kubainisha kuwa nchi hiyo imekuwa ikitoa misaada kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.

Dkt. Mwamba alibainisha kuwa misaada hiyo imekuwa ikitolewa kwenye sekta za Maji, Afya, Uhifadhi wa Maliasili na Mazingira, Usimamizi wa Fedha za umma na Usawa wa Kijinsia ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kuleta maendeleo endelevu ya kiuchumi na ya kijamii nchini Tanzania.

Alisema miradi hiyo inaendana na Dira ya Taifa ya mwaka 2025 inayoishia mwisho wa mwezi Juni 2026 na pia inaendana na Dira mpya ya 2050 na Mpango wa Taifa wa tatu wa Maendeleo wa Miaka mitano wa kuanzia mwaka 2020/21-2025/26 ambao unaishia June 2026 na pia inaendana na mpango mpya wa Nne wa Miaka Mitano wa mwaka 2026/27-2030/31.

Alisema Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ipo tayari kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimaendeleo na Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani kwa maendeleo ya watu wake.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri alisema mradi huo umekuja katika wakati muhimu ambapo mabadiliko ya tabianchi pamoja na ukuaji wa haraka wa miji vinaongeza shinikizo katika rasilimali za maji.

Alisema utekelezaji wa mradi huo utaimarisha usimamizi wa rasilimali za maji unaozingatia mabadiliko ya tabianchi na kuboresha upatikanaji wa huduma za maji kwa uhakika, hivyo kuchangia ustawi wa wananchi na maendeleo endelevu ya kiuchumi katika maeneo husika.

Mhandisi Waziri alisema kuwa Wizara ya Maji itaendelea kuhakikisha utekelezaji wa mradi huu unafanyika kwa ufanisi, uwazi na kwa wakati, kwa kushirikiana na wadau wote ili kuhakikisha manufaa yake yanawafikia wananchi wa Tanzania.

Kwa upande wao, Naibu Balozi wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani nchini Tanzania, Bw. Manuel Muller na Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) nchini Tanzania, Bi. Vanessa Eidt, walisema kuwa Ujerumani ni mmoja wa washirika wakubwa wa maendeleo wa Tanzania, ikiwa na miradi ya zaidi ya euro milioni 400 inayotekelezwa kupitia misaada na ushirikiano wa kifedha huku Sekta ya maji ndiyo inayoongoza kwa kiwango cha uwekezaji, ikifuatiwa na sekta ya uhifadhi wa bayoanuwai, jambo linalodhihirisha umuhimu wa ushirikiano huu katika kuimarisha maendeleo endelevu nchini.

Walisema wanaamani kuwa wataendelea kufanya kazi pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kufikia malengo pamoja ya maendeleo jumuishi na endelevu.