Na Mwandishi Wetu,Dodoma
WAKALA wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) umesema umejizatiti kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa na upatikanaji wa uhakika wa mafuta wakati wote kupitia mfumo wa uagizaji wa pamoja, hatua inayochangia ukuaji wa uchumi na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza leo Agosti 7, 2026 katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Mwandisi wa Petroli wa PBPA, Rehema Adam Maundi, alisema taasisi hiyo inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake ya kusimamia na kuratibu mfumo wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja pamoja na mchango wake katika maendeleo ya taifa.

Alisema PBPA imeendelea kushindanisha zabuni za kimataifa na kuingia mikataba yenye tija kwa ajili ya uagizaji wa mafuta, jambo linalohakikisha nchi inakuwa na akiba na upatikanaji wa bidhaa hizo hata pale zinapotokea changamoto katika soko la kimataifa.
Aidha Maundi alifafanua kuwa mfumo wa uagizaji hufanyika kila mwezi kwa kuzingatia mahitaji ya mafuta ya miezi miwili ijayo kupitia utaratibu maalumu unaowezesha serikali kuwa na mikataba imara ya usambazaji wa mafuta kwa wakati.

Alisema utaratibu huo umeendelea kuimarisha shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo sekta za uchumi, usafirishaji na utalii ambazo zinategemea upatikanaji wa mafuta kwa uhakika.
Aidha, alisema PBPA imeendelea kujenga uhusiano mzuri na nchi jirani kwa kuwezesha mafuta yanayoagizwa kupitia mfumo huo kuhudumia pia mataifa yanayopakana na Tanzania, yakiwemo Congo, Uganda, Malawi na Zambia kupitia bandari za Tanzania.

Aliongeza kuwa mfumo huo umeongeza uwazi na uwajibikaji kwa kuwa serikali sasa ina takwimu sahihi za mafuta yaliyopo nchini, yanayoingia na yanayotarajiwa kuwasili, huku mchakato wa zabuni ukiendelea kufanyika kwa uwazi kila mwezi.
Aidha Maundi amewahimiza wananchi kutembelea banda la PBPA katika Maonesho ya Nanenane ili kujifunza zaidi kuhusu majukumu ya wakala huo na namna unavyochangia kuhakikisha upatikanaji wa mafuta ya kutosha kwa maendeleo ya Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.


