NIC YATOA AHUENI KWA WAKULIMA WANAOPATA MAJANGA KUPITIA BIMA YA KILIMO


Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAKULIMA na wafugaji nchini wamehimizwa kutumia bima ya kilimo na mifugo kama njia ya kujikinga dhidi ya hasara zinazotokana na majanga ya asili, magonjwa na changamoto nyingine zinazoweza kuvuruga uzalishaji na kipato.


Wito huo umetolewa na NIC Insurance katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dk. John Samwel Malecela, Dodoma, ikieleza kuwa matumizi ya bima yanaweza kuwasaidia wazalishaji kuendelea na shughuli zao hata wanapokumbwa na majanga.


Akizungumza kwenye maonesho hayo, Afisa Bima wa NIC Insurance, Aman Mollel, amesema bima ya kilimo inalenga kulinda uwekezaji wa wakulima dhidi ya majanga kama ukame, mafuriko, magonjwa ya mimea, wadudu, vimbunga na mvua ya mawe vinavyoweza kupunguza mavuno au kusababisha hasara kubwa.


Amesema mazao yanayoweza kukatiwa bima ni pamoja na mahindi, mpunga, maharage, pamba, korosho, kahawa, tumbaku, shayiri, alizeti na chai.


“Kilimo ni uwekezaji mkubwa. Bima inampa mkulima uhakika wa kuendelea na uzalishaji hata anapopata hasara kutokana na majanga yasiyoepukika,” amesema Mollel.


Amefafanua kuwa mkulima anayehitaji huduma hiyo anatakiwa kujaza na kusaini fomu ya maombi, kuwasilisha taarifa za gharama za uzalishaji kwa hekta pamoja na makisio ya thamani ya mazao na historia ya uzalishaji wake.


Mbali na bima ya mazao, NIC Insurance pia inatoa bima ya mifugo inayowalinda wafugaji dhidi ya hasara zinazotokana na vifo vya mifugo vinavyosababishwa na ajali, magonjwa, wizi au uchinjaji wa lazima unaoshauriwa na daktari wa mifugo.


Kwa mujibu wa Mollel, bima hiyo inahusisha ng’ombe wa maziwa, ng’ombe wa nyama, kuku na mbuzi, huku waombaji wakitakiwa kuwasilisha fomu ya maombi iliyosainiwa, ripoti ya ukaguzi kutoka kwa afisa mifugo pamoja na ratiba ya chanjo za mifugo.


Amesema kiwango cha ada ya bima hutegemea thamani ya mnyama au mifugo inayokatiwa bima pamoja na asilimia inayotumika kwa aina husika ya bima.


Ameongeza kuwa pamoja na kufidia hasara, bima huwapa wakulima na wafugaji fursa ya kuendelea kuwekeza kwa kujiamini na kurahisisha upatikanaji wa mikopo kutoka taasisi za kifedha kutokana na kuwa na kinga ya uwekezaji wao.