Na Mwandishi Wetu,Dodoma
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kupitia kampuni ya T-Pesa imezitaka kampuni, taasisi na vyama vya ushirika kutumia Mfumo wa Malipo kwa Mkupuo (Bulk Payment) ili kurahisisha malipo kwa wakulima na wanufaika wengine, huku ikipunguza matumizi ya fedha taslimu.
Akizungumza katika Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayoendelea kitaifa mkoani Dodoma, Afisa Mauzo kutoka Kitengo cha T-Pesa, Husna Bwasi, alisema mfumo huo unaiwezesha taasisi au chama kufanya malipo kwa watu wengi kwa wakati mmoja badala ya kumlipa kila mnufaika mmoja mmoja.

Alisema malipo yanayoweza kufanyika kupitia mfumo huo ni pamoja na mishahara, posho, gawio na mapato ya mauzo ya mazao kwa wakulima.
“Vyama vya ushirika vinaweza kupakia orodha ya wanufaika wengi kwenye mfumo, kisha mfumo ukachakata na kufanya malipo kwa wakati mmoja. Hii inarahisisha mchakato wa malipo na kupunguza ulazima wa kubeba fedha taslimu,” alisema Bi. Bwasi.
Aliongeza kuwa mfumo huo unawaruhusu wakulima kupokea fedha moja kwa moja kwenye simu zao bila kujali mtandao wanaoutumia.
Mbali na huduma hiyo, Bwasi alisema T-Pesa pia inatoa huduma ya Lipa Namba, inayowawezesha wafanyabiashara wakubwa na wadogo kupokea malipo kwa njia ya kidijitali.

Alisema huduma hiyo haina masharti magumu, ambapo wafanyabiashara wadogo wenye majina binafsi wanahitaji kuwa na kitambulisho pekee ili kusajiliwa na kupewa Lipa Namba ya kupokea malipo kutoka mitandao mbalimbali.
Bi Bwasi aliwataka wafanyabiashara na vyama vya ushirika kutembelea banda la T-Pesa katika Maonesho ya Nanenane ili kupata elimu na kujiunga na huduma hizo zinazolenga kuongeza ufanisi wa malipo na kuimarisha biashara kwa njia za kidijitali.


