UTAFITI WA MADINI KUFUNGUA FURSA MPYA ZA UWEKEZAJI AJIRA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Serikali imeongeza kasi ya utafiti wa madini nchini katika hatua inayolenga kufungua maeneo mapya ya uwekezaji, kuongeza ajira na mapato ya Serikali, huku wachimbaji wadogo wakitarajiwa kunufaika kwa kupata taarifa sahihi zitakazowasaidia kufanya uchimbaji wenye tija.

Akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Eng. Ally Samaje, alisema utafiti wa kijiosayansi ndio msingi wa maendeleo ya sekta ya madini kwa kuwa huwapatia wawekezaji na wadau taarifa muhimu kuhusu maeneo yenye rasilimali.

Alisema hadi sasa GST imekamilisha utafiti wa jiolojia kwa asilimia 98 ya eneo lote la Tanzania, huku utafiti wa kijiofisikia wa kiwango cha kawaida ukifikia asilimia 100, hatua inayorahisisha utambuzi wa maeneo yenye fursa za uwekezaji wa madini.

Kwa mujibu wa Samaje, utafiti wa kijiofisikia wa kina umefikia asilimia 16, lakini Serikali imeanza maandalizi ya kuupanua kupitia programu mpya za urushaji ndege katika maeneo yenye rasilimali nyingi za madini.

Alisema awamu ya kwanza itahusisha utafiti katika eneo linalokadiriwa kuwa asilimia 18 ya ukubwa wa nchi, hatua itakayoongeza kiwango cha utafiti huo hadi asilimia 34 baada ya kukamilika, huku mkandarasi wa kazi hiyo akiwa tayari amepatikana.

Aliongeza kuwa awamu inayofuata itafanyika katika maeneo ya katikati ya Tanzania yenye ukubwa wa takribani asilimia 19 ya nchi, jambo litakalowezesha kufikia zaidi ya asilimia 50 ya utafiti wa kijiofisikia wa kina kabla ya mwaka 2030.

Samaje alisema GST pia imefikia asilimia 24 ya utafiti wa kijiokemia na mwaka huu wa fedha taasisi hiyo itafanya tafiti katika maeneo 18 mapya ili kuongeza kiwango hicho hadi asilimia 30.

Alisema maeneo mengi yaliyochaguliwa yana shughuli za uchimbaji mdogo, hivyo taarifa zitakazopatikana zitawasaidia wachimbaji kufanya kazi kwa uhakika badala ya kubahatisha, kuongeza uzalishaji na kuboresha kipato.

Mbali na hilo, alisema taarifa za tafiti zitawarahisishia wachimbaji wadogo kupata mikopo kutoka taasisi za fedha, huku GST ikiwa tayari kuthibitisha matokeo ya tafiti hizo ili kuongeza imani ya wakopeshaji.

Alisema utekelezaji wa programu hizo unafadhiliwa na Mfuko wa Utafiti wa Madini unaotokana na fedha za retention zinazokusanywa kupitia sekta ya madini.

“Upatikanaji wa taarifa sahihi za kijiosayansi utapunguza hatari kwa wawekezaji, kuongeza uwekezaji katika utafti na uchimbaji wa madini, kuchochea uanzishaji wa migodi mipya na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” alisema Samaje.