WAKULIMA WAKUMBUSHWA KUDAI FIDIA ZA BIMA KUPITIA MSULUHISHI BADALA YA MAHAKAMA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAKULIMA waliokata bima kupitia benki na mawakala wa bima wametakiwa kufahamu haki zao na kutumia Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima (TIO) kudai fidia wanapokumbana na migogoro, badala ya kukimbilia mahakamani.

Wito huo umetolewa na Msuluhishi Mkuu wa Migogoro ya Bima, Aloyce Mbunito, wakati wa Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.

Mbunito alisema ofisi hiyo, iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria Sura ya 394, inalenga kutatua migogoro ya bima kwa njia mbadala wa mahakama ili kurahisisha wananchi kupata haki zao kwa haraka na kuongeza imani katika sekta ya bima.

Alisema migogoro mingi inayowasilishwa ofisini hapo inahusisha kukataliwa kwa madai ya fidia, kucheleweshwa kwa malipo, kulipwa fidia isiyolingana na hasara halisi pamoja na kutokuelewana kuhusu masharti ya mikataba ya bima.

“Tangu kuanza kwa ofisi hii mwaka 2025 tumepokea na kufanikiwa kutatua migogoro zaidi ya 2,015. Hii inaonyesha wananchi wanaanza kutambua kuwa wana mahali pa kupata haki zao wanapokumbana na changamoto za bima,” alisema.

Alisema katika maonesho hayo walikutana na viongozi wa vyama vya ushirika kutoka Mkoa wa Mara waliowasilisha changamoto za wakulima wa tumbaku waliopata hasara kutokana na mvua ya mawe, licha ya kuwa walikuwa wamekata bima kupitia benki.

Kwa mujibu wa Mbunito, changamoto kubwa ni kwamba baadhi ya wakulima hawajui kampuni za bima zilizowahudumia kwa sababu walikata bima kupitia benki zilizokuwa mawakala wa bima, huku wengine wakikosa nakala za mikataba ya bima zinazohitajika wakati wa kufuatilia madai ya fidia.

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mara (WAMACU), Momanyi Range, alisema elimu waliyoipata imewasaidia kutambua umuhimu wa kuhifadhi mikataba ya bima na vielelezo vya hasara, ikiwemo kupiga picha za mazao yaliyoharibiwa na majanga.

Alisema chama hicho kimeanza kuhamasisha wakulima wote walioathirika kukusanya malalamiko yao, kupata nakala za mikataba kutoka benki husika na kuwasilisha madai yao katika Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima ili waweze kupata fidia stahiki na kurejea katika shughuli za uzalishaji.