Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kimeendelea kudhihirisha uwezo wake wa kuandaa wataalamu mahiri wa sekta ya bahari wanaoweza kushindana kimataifa, baada ya wanafunzi wake wawili wa kike kuwa miongoni mwa wanafunzi watano waliofanya vizuri zaidi na kutunukiwa Tuzo za Utendaji Bora (Best Performance Awards) katika Programu ya Kimataifa ya Mafunzo kwa Vitendo Melini (Smart Integrated Global On-Board Training Program 2026) nchini Korea Kusini. Programu hiyo ilihusisha washiriki 39 kutoka nchi 11, zikiwemo Tanzania, Kenya, Meksiko na Fiji. Miongoni mwa washiriki hao walikuwa wanafunzi wanne kutoka DMI, Tanzania. Hii ni awamu ya nne kwa Chuo kushiriki katika programu hiyo kuanzia mwaka 2023.
Akizungumza katika hafla ya kuwapokea wanafunzi hao, iliyofanyika tarehe 27 Novemba 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa DMI, Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana, Mhandisi Mkuu Paul Olekashe, aliupongeza Uongozi wa Chuo, Menejimenti, wakufunzi na watumishi wote wa Chuo kwa juhudi za kuboresha elimu na mafunzo ya mabaharia.

Mhandisi Olekashe alisema kuwa mafanikio hayo ni kielelezo cha ubora wa elimu na mafunzo yanayotolewa na DMI. Alisisitiza umuhimu wa kuweka kumbukumbu na kutangaza mafanikio ya Chuo ili jamii na wadau wafahamu mchango wake katika maendeleo ya sekta ya bahari na uchumi wa buluu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo Profesa Tumaini Gurumo aliwapongeza wanafunzi wote walioshiriki katika programu hiyo kwa nidhamu, ushirikiano na juhudi walizoonesha, akibainisha kuwa mafanikio ya wanafunzi waliotunukiwa tuzo yalitokana na juhudi za pamoja za kundi zima.

Aliwataka wanafunzi hao kuwashirikisha vijana wenzao maarifa na uzoefu walioupata, hususan kuhusu matumizi ya teknolojia ya akili unde (Artificial Intelligence – AI) na kujitafutia maarifa zaidi ya yale wanayopata darasani. Vilevile, aliwahimiza kuendelea kufanya bidii katika kila fursa wanayoipata na kutumia ujuzi kwa ukuaji wao katika sekta na maendeleo ya Taifa.
Aidha, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa uwekezaji katika miundombinu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa vitendo. Alisisitiza umuhimu wa kuongeza na kuboresha vifaa hivyo ili kukidhi mahitaji yanayotokana na ongezeko la idadi ya wanafunzi na kuhakikisha wanapata umahiri unaohitajika katika sekta ya bahari.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Amina Samwel Tupa alisema kuwa programu hiyo iliwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa mafunzo kwa vitendo yanayowawezesha kutumia vifaa, mitambo na mashine halisi ili kukamilisha maarifa na ujuzi wanaopata darasani na kupitia mifumo ya uigaji yaani Simulation Systems.



