TAMISA YAWATAKA WATANZANIA KUCHANGAMKIA FURSA SEKTA YA MADINI

Na Aziza Masoud,Dar es Salaam

WATANZANIA wametakiwa kuchangamkia fursa katika sekta ya madini ili waweze kunufaika kupitia majukwaa mbalimbali yakiwemo ya nje ya nchi.

Akizungumzia na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Machi 14, 2025 Mwenyekiti wa Kamati ya Kamati ya Masoko na Mawasiliano wa Chama cha Wasambazaji wa Sekta ya Madini Tanzania (TAMISA),Dk. Sebastian Ndege katika kuelekea uzinduzi wa kamati  ya chama hicho utakaofanyika Mei 16 mwaka huu ambao utaenda sambamba na kongamano la wadau wa sekta ya madini wameona ni wakati wa Watanzania kufahamu fursa zilizopo katika eneo hilo muhimu kwa Taifa.

“Chama hiki ni muhimu kwa Watanzania watu wengi hawajui sekta ya madini kama kuna fursa,lengo letu sisi no kutaka watu wafahamu kuwa kuna nafasi na  fursa mbalimbali katika sekta ya madini,”alisema Ndege.

Alisema kupitia kongamano hilo pia wadau watafanya matukio mbalimbali ikiwemo  majadiliano kuhusu nafasi ya wazawa kwenye utoaji  huduma katika sekta ya madini.

“Tunafahamu kwamba kuna changamoto nyingi kwenye ushiriki wa watu wa kawaida katika sekta ya madini kwakuwa ni huduma inayohitaji mtaji mkubwa,lengo lakuanzia hii ni kuonyesha kwamba hata ukiwa na mtaji mdogo unaweza kufanya biashara,”alisema Ndege.

Alisema kama hiyo ya TAMISA itazinduliwa na Waziri wa Madini,  Anthony Mavunde.

“Tunafahamu sisi Watanzania madini ni ya kwetu, na tunafahamu ya kuwa tunakila sababu ya kushiriki katika uchumi wa madini na Serikali yetu pamoja na Waziri wetu Mhe. Mavunde amekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha ushiriki wa Watanzania katika sekta hii,” alisema Dkt. Ndege.

Kwa upande wake Mwenyekiti TAMISA  Kumalilwa amesema Waziri Mavunde amekuwa akiongelea kuwa katika sekta hii ya madini kuna kiasi cha shilingi trilioni 3.1 ambayo inatumika kila mwaka katika manunuzi ambayo angependa Watanzania wanufaike nayo.

“Kuna migodi mikubwa nchini kama mitano, ambayo wao kila mwaka wanafanya manunuzi ya shilingi trilioni 3.1, ambapo sisi Watanzania tunanufaika kwa karibu asilimia 10 tu, kiasi hiki ni kidogo sana,” amesema Kumalilwa.

Amesema kwa kutambua hilo TAMISA imeweka mikakati ya kuhakikisha Watanzania zaidi wanaanzisha viwanda vya madini na kushiriki kikamilifu katika sekta hiyo ili kuweza kunufaika japo na asilimia 30 ya kiasi cha hicho shilingi trilioni 3.1 za manunuzi ya sekta ya madini.

“Kwa sasa hivi sisi Tanzania tunasheria ya local content, kwa wakati wangu kama Mkwenyekiti wa TAMISA nitahakikisha Watanzania wananufaika na shilingi trilioni 3.1 za manunuzi japo kwa asilimia 20 hadi 30,” alisema Kumalilwa na kuongeza,

“Tumekuwa tukilalamika sana kuhusu Wachina wanakuja nchini wanachukua kazi zetu, sasa sisi kama TAMISA tumekuwa tukihakikisha kwamba tunawajengea uwezo Watanzania ili waweze kushiriki katika uchumi wa sekta ya madini nchini,” alisema Kumalilwa.

TAMISA iliyozinduliwa Septemba 15, 2024 na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, inamalengo makuu ya kutetea wasambazaji wa sekta ya madini, kuboresha uwezeshaji wa biashara, kutetea haki za wasambazaji na kuendeleza utafiti na ukuaji wa teknolojia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *