BABA LEVO ATEMBELEA BANDA LA TTCL

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

MSANII na Mtangazaji maarufu nchini ambaye pia ni Balozi wa Kampeini ya Walete ya Shirika la Mawasiliano Tanzania -TTCL, Clayton Revocatus Chipando, maarufu kama Baba Levo ametembelea banda la TTCL katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya SabaSaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Baba Levo ametumia nafasi hiyo kuzungumza na wateja, kuhamasisha matumizi ya huduma za TTCL na kueleza namna Shirika hilo la Umma lilivyo kiungo muhimu katika kuleta mapinduzi ya kidigitali nchini na kutoa pongezi kwa juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha shirika hilo linabaki kuwa mhimili wa mawasiliano nchini.

Ziara hiyo ya Baba Levo imekuwa kivutio kikubwa kwa wananchi na mashabiki waliokusanyika kwa wingi kushuhudia msanii huyo akiungana na watumishi wa TTCL katika kutoa elimu kuhusu huduma na bidhaa zinazotolewa na shirika hilo la kihistoria.

Amesema kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari serikali imeliwezesha shirika hilo kutekeleza majukumu yake kama mtoa huduma wa msingi wa mawasiliano nchini. 

“TTCL ni alama ya Taifa.

 Tunapaswa kujivunia kuwa na taasisi ya kizalendo inayohakikisha mawasiliano ya Watanzania yanakuwa salama, ya uhakika na ya gharama nafuu,” alisema Baba Levo.

Katika mazungumzo yake na wataalamu wa TTCL waliopo sabasaba, msanii huyo alionesha kufurahishwa na maendeleo ya kiteknolojia yanayofanywa na shirika hilo, ikiwemo usambazaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, Kituo cha kuhifadhi Data Kimtandao, huduma ya intaneti ya kasi kwa wananchi, huduma za simu, pamoja na bidhaa za kisasa kama vile modemu, MiFi na huduma ya faiba mlangoni inayowezesha vifaa vya vifaa vya nyumbani kutumika kidigitali.

Kwa upande wake, Meneja wa Banda ambaye pia ni Meneja Bidhaa, Janeth Maeda, alisema ujio wa Baba Levo katika banda hilo unaashiria kuungwa mkono kwa taasisi za umma na wasanii wenye ushawishi mkubwa katika jamii.

“Tunamshukuru Baba Levo kwa kutenga muda wake kututembelea. Hii ni ishara kuwa jamii inatambua umuhimu wa TTCL kama taasisi ya umma inayotekeleza dhamira ya Serikali ya kuwafikishia Watanzania wote huduma za mawasiliano,” alisema Maeda.

Maonesho ya mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo “Maonesho ya Biashara ya Kimataifa – Sabasaba, Fahari ya Tanzania’’ TTCL imeiendeleza kwa kuonesha namna huduma zake zinavyounga mkono ajenda ya kidijitali ya taifa na uwekezaji katika sekta ya mawasiliano huku ikiwahakikishia wateja wake usalama, ubora na unafuu wa gharama.