Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
MAHAKAMA Kuu ya Uhujumu Uchumi, Divisheni ya Makosa ya Rushwa, imemhukumu kifungo cha miaka 28 jela mshtakiwa David Kanayo Chukwu, raia wa Nigeria, ambaye ni mshtakiwa wa kwanza kati ya watatu, baada ya kukiri kosa la kushiriki katika kusafirisha kilogramu 268.50 za dawa za kulevya aina ya heroin.
Akisoma hukumu hiyo Januari 22, 2026, Hakimu Otaru Joachimu alisema kuwa mahakama imezingatia miaka 5 na miezi 9 aliyokaa gerezani mshtakiwa huyo tangu alipokamatwa. Hivyo basi, atatumikia kifungo cha miaka 22 na miezi mitatu iliyobaki ili kukamilisha adhabu yake.

Aidha, mahakama hiyo imemuondolea mashtaka Alistair Amon Mbele, ambaye ni mshtakiwa wa tatu, baada ya Jamhuri kushindwa kuthibitisha hatia dhidi yake katika shauri namba DCEA/IR/06/2020 ECO 36/2020 linalowahusu David Kanayo Chukwu (raia wa Nigeria), Isso Lomward Lupembe (Mtanzania), na Alistair Amon Mbele (Mtanzania).
Kwa upande wa mshtakiwa wa pili, Isso Lomward Lupembe, kesi yake inaendelea katika mahakama hiyo baada ya kukana shtaka linalomkabili.

Vilevile, mahakama imeagiza kuwa shauri la jarada la mali za watuhumiwa hao (asset forfeiture) linapaswa kushughulikiwa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kuanzia tarehe ya kusomwa kwa hukumu hiyo.
Watuhumiwa hao walikamatwa na maafisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) mwaka 2020 eneo la Mbezi kibanda cha mkaa, wakituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya kiasi cha kilogramu 268.50 aina ya heroin.

Shauri hilo limeahirishwa hadi tarehe 23 Februari, 2026, litakapopangwa kusikilizwa tena.


