- Mume alitoweka Aprili 30 akaokotwa Mei 9 mwaka huu Pori la Mpoloto akiwa ameuawa
- Mara ya mwisho alionekana na mkewe wanakwenda kwa mganga huku wamepakiwa na anayedaiwa kumuua
Na Mwandishi Wetu, Songwe
WANANCHI wa Kijjiji cha Isongole, Wilaya ya Ileje mkoani Songwe bado wapo kwenye taharuki wasijue nini kimetokea baada ya mwanakijiji mwenzao kukutwa ameuwawa katika mazingira ya kutatanisha huku mkewe akiwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji.
Kwa mujibu wa taarifa, hadi jana Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limekuwa likiendelea na uchunguzi juu ya kifo cha Victor Mwakapenda (41) huku watu wawili wameshikiliwa na jeshi hilo wakati uchunguzi ukiendelea juu ya kifo hicho cha utata.
Wanaoshikiliwa ni mke wa marehemu na dereva wa Bodaboda ambaye anadaiwa kuwa ni hawara wa mke huyo, ambao majina yao yamehifadhiwa ili kutovuruga uchunguzi.
Aidha, kwa taarifa zilizopo kutoka kwa wanakijiji mke wa marehemu ni mtumishi Idara ya Afya, mkoani Songwe, ambapo inadawa walishirikiana na hawara yake kupanga njama ya kufanya mauaji ili wapate uhuru wa kufaidi penzi lao jipya.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augostino Senga alisema marehemu Victor Mwakapenda (41) mkazi wa Mtaa wa Ilembo alikutwa ameuawa na watu wasiofahamika na mwili wake kutupwa kwenye Pori la Mpoloto lililopo Mbeya Vijijini.
“Marehemu alitoweka nyumbani tangu Aprili 30 mwaka huu wakiwa na mke wake, ndugu zake walimtafuta bila mafanikio lakini Mei 9 mwaka huu aliokotwa akiwa amefariki dunia katika Msitu wa Mpoloto, Kijiji cha Igale Wilaya ya Mbeya Vijijini huku mwili ukiwa na majeraha usoni, kichwani na maeneo mbalimbali,” alisema Kamanda Senga.
Alibainisha kuwa, awali wananchi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi hawakujua kama mwili huo ni wa Victor ambapo ulipelekwa Hospitali ya Ifisi jijini Mbeya kwa ajili ya kuuhifadhi hadi ndugu walipoutambua Mei 29 mwaka huu na kukabidhiwa kwa ajili ya mazishi. Alizikwa kijijini Isongole wilayani Ileje mkoani Songwe.
“Kwa sasa tunawashikilia watu wawili ambao inadaiwa walikuwa na mahusiano ya kimapenzi, siku ambayo marehemu alitoweka nyumbani dereva bodaboda ambaye inadaiwa alikuwa mpenzi wa mke wa marehemu aliwabeba marehemu na mke wake akiwapeleka kwa mganga,” alisema Kamanda Senga.
Akitaja chanzo cha mauaji hayo, Kamanda Senga alisema mwanamke alimueleza mumewe waende kwa mganga wa kienyeji ili wakanywe dawa, kwani muendesha bodaboda huyo alimpa dawa akatapishwe.
Wakiwa njiani katika maeneo ya Senjele walitokea watu wawili wasiofahamika walisimamisha pikipiki hiyo na kumchukua marehemu huku wakiwaeleza mwananke na muendesha bodaboda warudi walikotoka kisha wakatoweka na marehemu.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa za Jeshi la Polisi wakiwa njiani kabla hawajavamiwa na hao watu waliotoweka naye marehemu alipata wasiwasi juu ya usalama wake akatuma ujumbe kwa ndugu zake na kuandika namba za Pikipiki waliyopanda huku akisema lolote likitokea wawe makini na pikipiki hiyo, hali hiyo ilirahisisha kukamatwa kwao.
Baada ya kupokea ujumbe huo, ndugu zake walitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kwa kuonesha ujumbe wa simu uliotumwa na marehemu, baada ya tukio la kupotea Victor, Polisi walimsaka dereva bodaboda na kumkamata pamoja na mwanamke huyo.
”Tumewashikilia watu hawa wawili na bado tunaendelea kuwasaka wauaji, pia vitendo hivi havikubaliki ndani ya jamii, hivyo Jeshi la Polisi halitasita kuwakamata watu wanaovunja sheria kwa kutoa uhai wa watu wengine kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kimapenzi,” alisema.
Akizungumza na mwananchi katika maziko hayo, Balozi wa Shina Namba 1 katika mtaa aliokuwa akiishi marehemu, Aliki Songa alisema:
“Tunasikitika kwa mauaji ya mwenzetu, kifo chake kinahusishwa na wivu wa mapenzi. Amekufa bila hatia kwa sababu ya tamaa za kidunia.
“Tunashukuru Jeshi la Polisi kuwashikilia watu hawa kwani sisi kama wananchi hatujawahi kushuhudia tukio la namna kama hili, hivyo kama unaona umechoka kukaa na mwenzako bora uachane naye kuliko kusababisha kifo ni mbaya sana.”
Baadhi ya majirani walisema mwanamke alionyesha kumchoka mumewe hadi kufikia hatua ya kutafuta hawara (dereva bodaboda), mapenzi yalivyozidi kunoga wakafikia hatua ya kupanga njama hizo mbovu ili wafaidi penzi lao jipya.