Unahusisha Shule za Sekondari 52 na Chuo kimoja cha VETA
Ni sehemu ya mradi wa Shilingi bilioni 25.8 wa kupeleka nishati safi ya kupikia kwa taasisi 453
Na Mwandishi Wetu,Dodoma
NAIBU Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amezindua awamu ya kwanza ya mradi wa kusambaza nishati safi ya kupikia katika taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100, unaohusisha shule 52 za sekondari pamoja na chuo kimoja cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika mikoa 18 ya Tanzania Bara.
Mradi huo ni sehemu ya mpango mkubwa wa kuunganisha miundombinu ya nishati safi ya kupikia katika taasisi 453 wenye thamani ya Shilingi bilioni 25.8, ambapo gharama zote zinagharamiwa kwa asilimia 100 na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Mhe. Salome Makamba amezindua mradi huo tarehe 17 Februari 2026 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kondoa, mkoani Dodoma, ambayo imekuwa taasisi ya kwanza kufungiwa mfumo wa nishati safi ya kupikia kupitia mradi husika.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Salome amesema kuwa mradi unahusisha usimikaji wa mifumo ya gesi ya LPG, ufungaji wa majiko banifu pamoja na usambazaji wa mkaa mbadala katika taasisi 453.

Ameeleza kuwa katika awamu ya kwanza, taasisi 53 zitanufaika, huku awamu ya pili ikihusisha taasisi 400 zilizopo katika mikoa yote nchini.
Ametanabaisha kuwa, kuwepo kwa mradi huo ni utekelezaji wa azma ya Serikali inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya 100 zinatumia nishati safi ya kupikia.

“Ili mradi huu uwe endelevu, nitoe wito kwa Serikali za Mitaa, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na TAMISEMI kusimamia mifumo iliyofungwa ili iwe endelevu suala litakalohamasisha jamii kuiga mfano wa taasisi za umma kuhamia katika nishati safi ya kupikia.” amesema Mhe. Salome
Aidha, ameitaka sekta binafsi kuona na kuchangamkia fursa iliyopo katika uzalishaji na usambazaji wa nishati safi ya kupikia ili kuongeza upatikanaji na kupunguza gharama kwa wananchi.

Vilevile, Mhe. Salome ameitaka REA kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia katika maeneo ya minada, stendi na masoko. kwani tafiti zinaonesha kuwa kuna minada ya awali na upili ipatayo 13,763 pamoja na masoko ya samaki yapatayo 1,229 nchini, ambayo yanapaswa kufikiwa kutokana na kuhudumia kundi kubwa la wananchi.
Vilevile, amesisitiza uwekaji wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia katika shule zote za umma na binafsi ili kutimiza azma ya Serikali kwa taasisi zinazohudumia zaidi ya watu 100 kutumia nishati hiyo.

Kwa walimu na wanafunzi, ametoa wito wawe mabalozi wa mabadiliko kwa kuanzisha klabu za nishati safi ya kupikia shuleni ili kupeleka ujumbe huo katika familia na jamii zinazowazunguka.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Jonas Mbunda, amemshukuru Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha na kugharamia mpango wa nishati safi ya kupikia, akieleza kuwa unalinda afya za wananchi na mazingira.

Naye, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ambaye ni Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia, Nolasco Mlay, amesema mradi huo utapunguza matumizi ya kuni na mkaa katika taasisi za elimu, kuchangia uhifadhi wa mazingira, kuboresha afya na usalama wa wapishi pamoja na kuongeza ufanisi wa uendeshaji wa shule.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Jones Olotu, amesema takwimu zinaonesha kuwa matumizi ya nishati isiyo safi yamepelekea takribani hekta 46,606 za misitu kuharibiwa kila mwaka kwa ajili ya kuni na mkaa, watu zaidi ya 33,000 wakifariki kutokana na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia na wanawake na watoto wa kike kutumia saa 4 hadi 8 kutafuta kuni, jambo linaloathiri muda wa shughuli za maendeleo.
Amesema Serikali ilitambua changamoto hizo na hivyo kuja na mkakati wa nishati safi ya kupikia ili kulinda mazingira, afya na muda wa kufanya shughuli za maendeleo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia za Nishati Mbadala kutoka REA, Mhandisi Advera Mwijage, amesema mradi wa nishati safi ya kupikia katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kondoa umegharimu Shilingi milioni 54.
Amesema katika shule hiyo, limefungwa tanki la gesi lenye ujazo wa tani moja linaloweza kuhudumia upishi kwa takribani miezi miwili, pamoja na mfumo wa mkaa mbadala unaotokana na mabaki ya miwa.
Mkuu wa shule hiyo, Mwl. Flora Nusu, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa mradi huo, akieleza kuwa utaondoa athari za kiafya kwa wapishi na muda uliokuwa ukipotea katika kutafuta kuni, na pia kupunguza gharama za uendeshaji kwa asilimia 40.


