Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa leo tarehe 24 Februari, 2026 amekagua utekelezaji wa Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) Lot 5 kipande cha Mwanza–Isaka (km 341) unaogharimu Sh trilioni 3.06, na kuagiza kasi iongezwe huku viwango na ubora wa kimataifa vilivyosanifiwa kwa mtandao mzima wa SGR vikizingatiwa kikamilifu.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kugharamia mradi huo uliokuwa asilimia 0 ilipoingia madarakani na sasa umefikia asilimia 68.

Amesisitiza kuwa uwekezaji huo Mkubwa unalenga kuchochea ukuaji wa uchumi, kupunguza gharama za usafirishaji na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafiri Afrika Mashariki na Kati na kulitaka Shirika la Reli Tanzania (TRC) na wakandarasi kuongeza nguvu kazi na mitambo ili kukamilisha kazi zilizosalia kwa wakati na thamani halisi ya fedha,
Waziri Mbarawa, amebainisha kuwa usanifu wa reli umezingatia uwezo wa kubeba mizigo mikubwa, kasi ya juu ya treni na uimara dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi na kuwataka wananchi wa pembezoni mwa mradi kuulinda mradi na kujiandaa kikamilifu kutumia fursa zitakazojitokeza.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mha. Machibya Masanja, amesema utekelezaji wa jumla wa mradi huo umefikia asilimia 68 ,madaraja asilimia 90 na utandikaji reli asilimia 53, huku kazi za tuta, makalavati, madaraja na miundombinu ya vituo zikiendelea kuratibiwa na kuongeza kuwa lengo ni ifikapo 2028 treni ya kisasa isafiri kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.
Awali, Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe. Johari Samizi ameahidi ushirikiano wa mkoa katika kuusimamia na kuulinda mradi na kusisitiza kuwa maeneo ya kimkakati yatapangwa kwa manufaa ya wananchi na Serikali na kuwaasa wananchi kuonesha ushirikiano.









