Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
“Tunapokutana na marafiki tunakumbushana kwenda kanisani pamoja, lakini wazazi wetu hawafahamiani sana. Nimefundishwa kuwa makini na watu nisio wajua na kuepuka maeneo hatarishi kama vichaka. Nikihisi mtu ananitia wasiwasi nitatoa taarifa kwa watu wazima au polisi,” hii ni sauti ya mtoto Nick Edward mwenye umri wa miaka tisa.
Si ishara nzuri. Kwa sababu Nick amesema anasoma katika Shule ya St. John Bosco iliyopo Kibaha, lakini anaishi Kata ya Kiluvya takriban umbali wa kilomita 20. Ana marafiki 10 ambao wote wazazi wao hawawajui wala wazazi hawafahamiani.
Ingawa anakiri wazazi wake wamemfundisha kuwa makini na mwangalifu wakati wote awapo barabarani.
Kwa upande wake, Joan Denis Sentonga mwenye umri wa miaka 10 ni mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya St. John Bosco Kibaha-Tumbi, amesema walimu na wazazi wamekuwa mstari wa mbele kuwafundisha watoto umuhimu wa kujilinda.

“Tunafundishwa kuwa waangalifu kila tunapokuwa nje ya nyumba. Mimi mara nyingi hutoka nikiwa na mzazi au mtu ninayemwamini. Elimu hii inatusaidia kutambua mazingira salama na hatarishi,” amesema.
Mwandishi wa Makala haya alitembelea nyumba ya ibada ambako Watoto wenye umri chini ya miaka 10 wanapata mafunzo ya kiroho. Akakutana na kiongozi wa kiroho Katekista Geophrey Mrope.
Ni katika Kigango cha Mtakatifu Teresa wa Kalkuta kilichopo Parokia ya Watakatifu Wote Kiluvya, ambako kulikuwa na mafunzo ya watoto wanaojiandaa kupokea Sakramenti ya Ekaristi kwa mara ya kwanza.
Katekista Mrope ameeleza namna anavyowaelimisha kuhusu kujilinda dhidi ya vitendo vya ukatili na watu wanaoweza kuwa hatari kwa usalama wao.
Katekista Mrope amesema kwa mwaka mmoja aliokuwa akihudumu katika eneo hilo hajawahi kupokea taarifa ya mtoto aliyefanyiwa ukatili, lakini anaona kuna mazingira yanayoweza kuongeza hatari kwa watoto.
“Hawa ni watoto wangu wa kwanza wa mafundisho katika kigango hiki na wanatarajiwa kupokea Sakramenti ya Ekaristi ya Kwanza tarehe 14 mwezi huu mwaka 2026.
Kwa kuwa wanatoka katika familia na mazingira tofauti, bado sijabaini changamoto kubwa ya moja kwa moja ya ukatili, lakini kuna mambo yanayohitaji uangalizi,” amesema.
Ameeleza kuwa baadhi ya watoto wanaishi mbali na eneo la kanisa kutokana na makazi mapya yanayoendelea kujengwa, jambo linalowalazimu kutumia usafiri wa pikipiki maarufu Bodaboda au kusubiri muda mrefu kabla ya kufuatwa na wazazi wao.
“Wakati mwingine mtoto anaishi na mzazi mmoja ambaye anakuwa kazini muda mwingi. Baada ya mafundisho analazimika kusubiri hadi mzazi afike au apelekwe nyumbani kwa usafiri wa bodaboda. Hili ni eneo linalohitaji tahadhari kwa sababu si rahisi kuwaamini watu wote,” amesema.
Mrope amesema changamoto nyingine huonekana kwa watoto wanaolelewa katika mazingira yasiyo na wazazi wao wote, wakiwemo wanaoishi na baba wa kufikia, mama wa kufikia, babu, bibi, mjomba au shangazi.
Kwa mujibu wake, watoto wa aina hiyo mara nyingi hukabiliwa na changamoto za kihisia na kijamii ambazo zinaweza kuathiri ustawi wao wa jumla.
“Ninaweza kutambua kwa kiasi fulani mtoto anayepitia changamoto au aliyefanyiwa ukatili kutokana na mwenendo na hali yake ya kisaikolojia. Hata hivyo, hadi sasa sijapata kesi ya moja kwa moja katika kundi langu,” amesema.
Kwa upande wao, watoto waliohojiwa wameonyesha kuwa wana uelewa wa msingi kuhusu namna ya kujitambua na kujilinda dhidi ya watu wenye nia mbaya.
Patrick Edward Musa mwenye umri wa miaka 11, mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Tondoroni iliyopo Kiluvya, amesema anaelewa kuwa ukatili ni kitendo chochote kinachoweza kumdhuru mtoto kimwili au kihisia.
“Sijawahi kuona wala kufanyiwa ukatili, lakini wazazi wangu hunikumbusha kuwa nikiona mtu nisiyemfahamu au anayenifuatilia, nibaki mbali naye na nitoe taarifa kwa mwalimu, jirani au mzazi,” amesema Patrick.
Mtoto mwingine, Lelisteon John mwenye umri wa miaka 10 anayesoma darasa la tano katika shule ya Fransalian Mission School iliyopo Kibaha Picha ya Ndege, amesema watoto wanaelimishwa kutotoka nje bila ruhusa ya wazazi au walimu.
“Tunaambiwa kuwa si kila mtu ni salama kwa watoto. Mtu akiwa ananifuatilia mara kwa mara au kunifanya nijisikie vibaya, nitatoa taarifa kwa wazazi, walimu, majirani au polisi,” amesema.
Kauli za watoto hao zinaonyesha kuwa elimu ya ulinzi wa mtoto inayotolewa nyumbani, shuleni na katika taasisi za dini ina mchango mkubwa katika kuwajengea uwezo wa kutambua viashiria vya hatari na kutafuta msaada mapema.
Mwandishi wa Makala haya alikutana na Polisi Kata ya Kiluvya, Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Marwa Mageka akiwa katika majukumu yake ya kutoa elimu ya ukatili kwa watoto katika Kanisa la Kiluvya, Kigango cha Mtakatifu Teresa wa Kalkuta.
Amesema ukatili unaanzia katika ngazi ya familia na ndiyo maana kazi yake kubwa anayoifanya ni kuzungumza na Watoto, wazazi na walimu bila kuwasahau viongozi wa dini.
“Kadiri watoto wanavyozidi kupata maarifa kuhusu haki zao na namna ya kujilinda, ndivyo uwezekano wa kupunguza vitendo vya ukatili dhidi yao unavyoongezeka, jambo linalochangia kujenga jamii salama na yenye ustawi kwa kizazi cha sasa na kijacho,” amesema Afande Mageka na kusisitiza:
“Kata hii ina shule saba za msingi ambazo ni za serikali, shule za binafsi zipo nyingi siwezi kuzihesabu. Lakini shule zote nimefika na watoto wanajijua kwa sababu kila mwezi ninakuwa na ratiba ya kutembelea shule kuwapa mafunzo watoto hadi katika nyumba za ibada makanisani na misikitini.”
Anabainisha katika mwaka mmoja aliokaa katika kata hiyo amebaini watoto wengi wanaofanyiwa vitendo vya ukatili ukienda nyumbani unagundua anaishi na mzazi mmoja hasa mama.
“Kuna kesi moja mama alimchoma kiganja mtoto wake, tulipomuita mama akasema mtoto ni mdokozi, tukamuuliza alifanya nini baada ya kugundua tabia ya mtoto wake. Akaanza kulia na kueleza shida zake za kimahusiano. Maana yake wakati mwingine wazazi chuki za wenza wao wanazihamishia kwa Watoto,” anasema Afande Mageka.
Anatoa mfano mwingine wa mtoto katika shule ya Msingi Tondoroni, mzazi alimchapa mtoto hadi akamsababishia majeraha.
“Walimu wakatuita. Tulipomfuata mzazi tukagundua mtoto anaishi na mama peke yake. Mzazi akasema mtoto wake ni kiburi, mdokozi, na akasema akili yake haiko sawa kwa sabau alishawahi pia kukojolea vyombo vya chakula. Tulipomdadisi mzazi tukagundua tatizo lipo kwa mzazi,” anasema Afande Mageka.
Aidha, Afande Mageka anweka wazi kuwa utaratibu alioanzisha kuzungumza na wazai, walezi na watoto umesaidia kupunuza matukio ya ukatili, ndiyo maana anabainisha matukio yote aliyoyataja yametokea mwaka jana 2025, mwaka huu hakujatokea hata tukio moja.
“Ushauri ninaoutoa kwa wazai wawe wanafuatilia mienendo ya watoto wao, waangalie namna wanavyokwenda shule na wanavyorejea nyumbani. Waangalie aina ya marafiki wanaoandamana nao lakini pia waangalie vipindi wanavyofuatilia kwenye runinga je vina maadili au wanapowapa simu wanaangalia kitu gani vinaendana na umri wao,” anasema Afande Mageka.

Mwandishi wa Makala haya akiwa na Polisi Kata ya Kiluvya, Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Afande Marwa Mageka wakati wa mahojiano.

