WAZAZI WASHIRIKIANE NA WALIMU KULINDA WATOTO DHIDI YA UKATILI


Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
MZAZI anapomkabidhi mtoto kwa mwalimu anakuwa na matumaini ya kurudishiwa akiwa salama, akiwa na maarifa na tabia njema zaidi ya alivyomuacha asubuhi.


Hata hivyo, nyuma ya sare za shule na tabasamu zao, baadhi ya wanafunzi hubeba majeraha ya kimwili na kihisia yanayosababishwa na vitendo vya ukatili wanavyokumbana navyo nyumbani, shuleni au katika jamii zinazowazunguka.
Pengine wakiwa njiani kurudi nyumbani au asubuhi wanapokwenda shuleni.


Wataalamu wa elimu na walimu wanasema shule zimeendelea kuwa sehemu muhimu ya kutambua na kukabiliana na vitendo hivyo kutokana na nafasi ya kipekee waliyonayo walimu katika maisha ya watoto.


Hadi mwaka 2024 takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kupitia ripoti ya Tanzania in Figures 2024, ambayo hutumia taarifa za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Tanzania Bara ilikuwa na Shule za Msingi 20,533 ambapo kati ya hizo za Serikali ni 18,055 na za binafsi: 2,478. Shule za Sekondari ni 6,269, kati ya hizo za Serikali ni 4,905 za biinafsi ni 1,364.


Hivi vyote ni vituo vinavyopokea wanafunzi kuanzia umri wa miaka mitano hadi miaka 18. Wote Watoto wakiwa na matarajio makubwa baadaye.


Hata hivyo, wapo watu wenye nia ovu wanaotaka kukatisha ndoto za Watoto hawa kwa kuwafanyia ukatili wa kila namna. Ukatili unaowatia hofu na kukata tamaa.


Mwalimu wa Rejoyce Pre and Primary School iliyopo Makurunge, Kiluvya mkoani Pwani, Abushehe Hemedi, anasema ukatili dhidi ya watoto unaweza kutokea hata ndani ya shule bila kutambuliwa mapema.


“Mtoto anaweza kupewa adhabu kali isiyoendana na umri wake au kuambiwa maneno makali yanayoumiza hisia zake. Wengine hudharauliwa kutokana na maumbile yao, uwezo wao darasani au hali zao binafsi. Hizi zote ni aina za ukatili ambazo wakati mwingine hupuuzwa,” anasema Mwalimu Hemedi.


Kwa mujibu wake, ukatili hauishii kwenye vipigo pekee. Kutompa mtoto huduma stahiki kwa wakati, kutomsikiliza au kumzuia kujieleza ni vitendo vinavyoweza kuathiri ukuaji wake wa kihisia na kisaikolojia.


Katika mazingira ya shule, walimu ndiyo watu wa kwanza wanaoweza kubaini mabadiliko ya tabia za watoto. Hata hivyo, jambo hilo huhitaji ukaribu na uaminifu kati ya mwalimu na mwanafunzi.


Mwalimu Mwanvita Juma wa Shule ya Msingi Kigilagila, Ilala jijini Dar es Salaam, anasema walimu wanapaswa kujenga mazingira ya upendo yatakayowawezesha watoto kueleza changamoto zao kwa uhuru.


“Ukiwa karibu na mwanafunzi na ukamwonyesha unamjali, inakuwa rahisi kwake kukueleza matatizo anayopitia. Pia ukifuatilia mwenendo wake wa kila siku unaweza kugundua mapema kama kuna changamoto inayomkabili,” anasema Mwalimu Mwanavita.


Anataja baadhi ya dalili za mtoto anayepitia ukatili kuwa ni pamoja na utoro wa mara kwa mara, mabadiliko ya ghafla ya tabia, kukosa kujiamini, kuwa mnyonge bila sababu za msingi na kushuka kwa kiwango cha ufaulu darasani.


Naye mwalimu wa Fizikia na Hisabati wa Shule ya Sekondari Hidya Sultan mkoani Kigoma, Shadhir Boimanda, anasema walimu wanapaswa kuwa zaidi ya wafundishaji na kuwa walezi wanaowafahamu wanafunzi wao kwa undani.


“Tunapaswa kutengeneza ukaribu na wanafunzi ili wajisikie huru kutueleza changamoto wanazopitia. Wakati mwingine hata kuwatembelea nyumbani kunaweza kusaidia kuelewa mazingira wanayoishi na changamoto zinazowakabili,” anasema Mwalimu Boimanda.


Kwa mujibu wa Boimanda, baadhi ya watoto wanaopitia ukatili huanza kujitenga, kushindwa kushirikiana na wenzao au kupoteza hamasa ya masomo.


“Ukiona mwanafunzi ambaye ghafla amebadilika kitabia, hataki kushirikiana na wenzake au matokeo yake yanaporomoka bila sababu za msingi, ni muhimu kufuatilia kwa karibu. Mara nyingi kuna jambo kubwa analopitia,” anasema Mwalimu Boimanda.
Mbali na jukumu la kutambua ukatili, walimu pia wanatajwa kuwa sehemu muhimu ya mfumo wa utoaji taarifa.


Mwalimu Hemedi anabainisha kuwa shule zinapaswa kuwa na mifumo madhubuti ya kuripoti matukio ya ukatili kupitia walimu wa nidhamu, walimu walezi, viongozi wa shule na klabu za watoto kama TUSEME Club.


Anasema baada ya taarifa kufikishwa shuleni, hatua zinazofuata zinapaswa kuhusisha mamlaka husika zikiwemo Ofisi za Ustawi wa Jamii, Dawati la Jinsia na Watoto la Jeshi la Polisi, maafisa elimu wa kata pamoja na matumizi ya namba ya dharura ya watoto 116.


“Cha muhimu ni kuhakikisha usiri wa mtoto unalindwa wakati wote. Jina lake lisitolewe hadharani na apewe msaada wa haraka wa matibabu, ulinzi na ushauri wa kisaikolojia,” anasisitiza Mwalimu Hemedi.


Pamoja na juhudi hizo, walimu wanakiri kuwa bado wanakabiliwa na changamoto nyingi katika kupambana na ukatili dhidi ya watoto.
Mwalimu Boimanda anasema wakati mwingine familia au walezi huingilia kati na kuzuia hatua za kisheria kuchukuliwa.


“Wapo wanaonufaika na mazingira hayo, hivyo wanapinga suala lisifikishwe kwenye vyombo vya sheria. Pia jamii nyingi bado hazina uelewa wa kutosha kuhusu ukatili wa watoto,” anasema Mwalimu Boimanda.


Kwa upande wake, Mwalimu Mwanvita anataja ukosefu wa ushirikiano kutoka kwa baadhi ya wazazi kuwa miongoni mwa changamoto kubwa zinazowakwamisha walimu kufuatilia kesi za watoto wanaodhaniwa kufanyiwa ukatili.


Mwalimu wa nidhamu katika Shule ya Msingi Chekelei iliyopo Korogwe mkoani Tanga, Juma Mohammed Kayemvya anasema kuna mabadiliko makubwa katika malezi ya Watoto.
“Wakati mwingine tunakuwa njia panda namna ya kukabiliana na changamoto hizi za ukatili wa watoto, hasa ukatili wa kijinsia. Kwa sababu wazazi wanakuwa wakali wanaposikia watoto wao wamepewa adhabu kutokana na makosa madogo madogo ambayo ndiyo msingi wa kurekebisha tabia zao.


“Ambacho walimu tunataraji ni kuona wazazi wanashirikiana nao kumtengeneza mtoto. Wanaposikia mtoto amepewa adhabu ambayo si ya kuumiza, wanatakiwa moja kwa moja wawasiliane na mwalimu kujua wapi mtoto ameteleza ili na yeye amrekebishe,” anasema Mwalimu Kayemvya.


Kutokana na hali hiyo, walimu hao wanasisitiza umuhimu wa kuimarisha elimu ya ulinzi wa mtoto kuanzia ngazi ya chekechea hadi sekondari.


Kwa mujibu wao, watoto wanapaswa kufundishwa namna ya kujitambua, kutambua hatari zinazowazunguka, kuelewa haki zao na kujua sehemu sahihi za kutoa taarifa wanapokumbana na vitendo vya ukatili.
Wanasema vita dhidi ya ukatili wa watoto haviwezi kuachiwa shule pekee. Ushirikiano wa wazazi, jamii, serikali na taasisi mbalimbali ni muhimu ili kuhakikisha kila mtoto anakua katika mazingira salama yanayomwezesha kufikia ndoto zake.


Kadiri jamii inavyoendelea kutambua athari za ukatili dhidi ya watoto, ndivyo inavyokuwa wazi kuwa mwalimu si mtoa elimu tu, bali ni mlinzi wa kwanza wa haki na ustawi wa mtoto.



Polisi Kata katika Kata ya Kiluvya, Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Afande Marwa Mageka akizungumza na watoto katika nyumba ya ibada ikiwa ni sehemu ya mkakati wake kuwafikia watoto na kuwapa elimu namna ya kujilinda dhidi ya ukatili.