VYOMBO VYA HABARI VINA NAFASI KULIPONYA TAIFA DHIDI YA UKATILI WA KIJINSIA


Na Mwandishi Wetu,Pwani
VYOMBO vya habari vina nafasi kubwa katika kuhamasisha usawa wa kijinsia, kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto, pamoja na kujenga jamii inayoheshimu haki za binadamu.
Hata hivyo, mafanikio ya juhudi hizi yanategemea kwa kiasi kikubwa namna habari zinavyokusanywa, kuandikwa na kuwasilishwa kwa kuzingatia misingi ya uandishi unaojali masuala ya jinsia.


Bado safari ni ndefu kwa Tanzania, kuna maeneo hayajafanyiwa kazi sawa sawa.
Takwimu za Kwa mujibu wa takwimu za kimataifa zinazotumia taarifa za Tanzania.


Kutoka tovuti ya UN Women Dat Hup kupitia United Republic of Tanzania Country Data Sheet, Tanzania ina asilimia 37.4 ya uwakilishi wa wanawake katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi mwaka 2024.


Aidha, taarifa hizo zinabainisha kuwa asilimia 29.1 ya wanawake wenye umri wa miaka 20 hadi 24 waliolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18, huku asilimia 24.3 ya wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49 wakiripoti kufanyiwa ukatili wa kimwili au kingono na wenza wao katika kipindi cha miezi 12 iliyopita, kwa maana hadi mwaka 2025.


Takwimu hizo pia zinaonyesha kuwa wanawake hutumia wastani wa asilimia 16.5 ya muda wao katika kazi zisizolipwa za malezi na shughuli za nyumbani ikilinganishwa na asilimia 4.2 kwa wanaume.


Mhariri wa Michezo wa Gazeti la Taifa Tanzania, Haroun Shehe Semtawa, anasema vyombo vya habari vina jukumu muhimu katika kuibua mijadala kuhusu usawa wa kijinsia, kutoa sauti kwa makundi ambayo hayajawakilishwa vya kutosha, kuelimisha jamii kuhusu haki za wanawake na watoto, pamoja na kupinga lugha na maudhui yanayodhalilisha jinsia yoyote.


“Vyombo vya habari vina nafasi ya kukuza uwajibikaji wa serikali na wadau mbalimbali katika utekelezaji wa sera za jinsia na kuhakikisha masuala haya yanapata uzito unaostahili katika jamii,” anasema Semtawa.
Anabainisha changamoto kadhaa katika uandishi wa habari unaozingatia jinsia.

Miongoni mwa changamoto hizo ni wanawake kuonekana mara chache katika vyanzo vya habari ikilinganishwa na wanaume, baadhi ya taarifa za ukatili wa kijinsia kuandikwa kwa lugha inayomlaumu mhanga, pamoja na uwakilishi mdogo wa wanawake katika nafasi za juu za maamuzi ndani ya vyombo vya habari.


Changamoto nyingine ni kuongezeka kwa taarifa potofu na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kupitia majukwaa ya kidijitali.


Kwa mujibu wa Semtawa, vyombo vya habari vinapaswa kuzingatia kanuni za uandishi unaojali jinsia kwa kuhakikisha uwakilishi sawa wa wanawake na wanaume, matumizi ya lugha isiyobagua na kutoa nafasi kwa makundi yote kushiriki katika mijadala ya maendeleo.


“Uandishi wa aina hii husaidia kupunguza ubaguzi, kuimarisha haki za binadamu na kuchochea maendeleo jumuishi nchini Tanzania,” anasisitiza Semtawa.


Kwa upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzana kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imeendelea kusimamia sera na mipango mbalimbali inayolenga kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto, kukuza usawa wa kijinsia, kuimarisha uwezeshaji wa wanawake kiuchumi na kushirikiana na wadau wa habari katika kampeni za uelimishaji wa jamii.


Mwaka 2024, Tanzania ilizindua Mpango wa Pili wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (2024/2025–2028/2029) unaolenga kuimarisha kinga dhidi ya ukatili, kuboresha huduma kwa waathirika na kuleta mabadiliko ya mitazamo katika jamii.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dodoma Mei 15, 2024, wakati huo akiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, anasema:


“Tunaposherehekea uzinduzi wa Mpango Kazi wa Pili wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto, tuna fursa ya kujitolea tena kulinda haki za kila mwanamke na mtoto nchini Tanzania. Wanawake na watoto wote wana haki ya kulindwa dhidi ya aina zote za ukatili.”


Anaongeza kuwa licha ya juhudi zinazofanyika, mamilioni ya wanawake na watoto nchini wamewahi kupitia au kushuhudia ukatili wa kimwili, kingono au kihisia, huku matukio mengi yakitokea katika maeneo yanayopaswa kuwa salama kama nyumbani, shuleni, mahali pa kazi, kwenye jamii na hata mtandaoni.


Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha ukubwa wa tatizo hilo. Waziri Gwajimba ameliambia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa vituo vya afya vilivyotoa huduma kwa waathirika vilirekodi jumla ya waathirika 108,819 wa ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto kati ya Julai 2025 na Aprili 2026. Kati ya hao, watoto wal

ikuwa 32,150 na watu wazima 76,669.
Kwa mujibu wa ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto pamoja na Viashiria vya Malaria Tanzania wa mwaka 2022 (TDHS-MIS 2022), asilimia 27 ya wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49 wamewahi kufanyiwa ukatili wa kimwili tangu walipofikisha umri wa miaka 15, huku asilimia 12 wakiripoti kufanyiwa ukatili wa kingono katika muda wote wa maisha yao.


Aidha, takribani mwanamke mmoja kati ya watatu nchini amewahi kupitia aina moja au zaidi ya ukatili wa kijinsia katika maisha yake.

Takwimu za Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) zilizochapishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha kuwa karibu asilimia 30 ya wanawake wa Tanzania Bara wenye umri wa miaka 15 hadi 49 wamewahi kufanyiwa ukatili wa kimwili tangu walipofikisha umri wa miaka 15.


Mwandishi wa habari mkongwe wa Gazeti la Habari Leo, Anastazia Anyimike, anasema vyombo vya habari vina jukumu la kuelimisha jamii, kuhamasisha mabadiliko ya tabia, kutoa taarifa sahihi na kufichua matukio ya ukatili wa kijinsia ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.


Hata hivyo, anabainisha kuwa habari za ukatili wa kijinsia haziandikwi kwa kiwango kikubwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo masharti ya kisheria na makatazo ya mahakama kwa angalizo la kutoingilia mwenendo wa kesi.


“Wakati mwingine taarifa zisizo sahihi zinaweza kumuathiri mwathirika kisaikolojia, kuvunja haki zake na hata kuathiri uchunguzi wa kesi husika,” anasema Anastazia.


Anataja sababu nyingine kuwa ni ukosefu wa taarifa sahihi, hofu ya waathirika kujitokeza hadharani, mila na desturi zinazoficha ukweli pamoja na ukosefu wa mafunzo maalumu kwa baadhi ya waandishi wa habari.


“Aina hii ya uandishi wa habari za ukatili wa kijinsia ni uandishi unaotoa nafasi sawa kwa jinsia zote, unaoheshimu haki za binadamu na kuepuka ubaguzi au unyanyapaa. Mwandishi anatakiwa kuzingatia usahihi wa taarifa, kulinda faragha ya mwathirika, kutumia lugha yenye heshima, kupata ridhaa inapohitajika na kuzingatia maadili ya taaluma,” anafafanua Anastazia.


Anasisitiza kuwa waandishi wa habari wanapaswa kuepuka lugha ya kulaumu waathirika, maelezo yanayodhalilisha utu wao na matumizi ya habari za kusisimua ambazo hazina mchango wa kielimu kwa jamii.


“Habari zinazoripotiwa kwa usahihi zina mchango mkubwa katika kuhamasisha vita dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa sababu huongeza uelewa wa jamii, huwahamasisha waathirika kutafuta msaada na kusaidia mamlaka kuchukua hatua stahiki,” anasema.


Kwa mujibu wake, waandishi wa habari wana nafasi ya kutoa elimu, kuibua mijadala ya kijamii na kuonesha athari za ukatili wa kijinsia kwa familia, jamii na taifa kwa ujumla.


Anasema ushiriki wa wanawake, wanaume, vijana na watoto katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia unaweza kuimarishwa kupitia vipindi vya redio na televisheni, mitandao ya kijamii, makala maalumu na mijadala inayowashirikisha wadau kutoka makundi mbalimbali ya kijamii.


Pia amependekeza waandishi wa habari kuendelea kupata mafunzo kuhusu maadili ya taaluma, haki za binadamu, usawa wa kijinsia, ulinzi wa watoto na mbinu za kufanya mahojiano na waathirika wa ukatili.


Mbali na hilo, anasisitiza kuwa vyombo vya habari vinapaswa kuandaa miongozo ya kitaaluma, kutoa mafunzo endelevu na kusimamia utekelezaji wa sera za usawa wa kijinsia mahali pa kazi ili kuhakikisha habari zinazotolewa zinachangia kujenga jamii yenye usawa, haki na maendeleo kwa wote.

Mwandishi wa Makala haya akiwa na wazazi na walezi katika Kijiji cha Chekelei, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga ambapo wametoa maoni juu ya haja ya kuwepo waandishi wa habari maalumu watakaojihusisha moja kwa moja na habari za ukatili wa kijinsia na ulinzi wa watoto.