Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umesema maboresho ya mfumo wake wa usajili yameongeza ufanisi, uwazi na usalama wa huduma za urasimishaji wa biashara, huku wananchi wakipata fursa ya kujifunza na kupata huduma hizo moja kwa moja katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea viwanja vya Mzunguni, Dodoma.
Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa Usajili wa BRELA, Yusuph Mwasakafyuka Regio, alisema mfumo mpya umeondoa changamoto zilizokuwapo katika mfumo wa awali wa ORS na kuruhusu huduma nyingi kufanyika kwa njia ya mtandao bila mteja kulazimika kufika ofisini.
Alisema kupitia mfumo huo, huduma kama usajili wa majina ya biashara, kampuni, leseni za biashara Kundi A, leseni za viwanda na usajili wa awali wa alama za biashara (Trademark) zinapatikana kwa urahisi zaidi.
Kwa mujibu wake, mfumo huo pia umeongeza uwazi kwa kuwawezesha wananchi kupata taarifa za kampuni, ikiwemo hali ya uwasilishaji wa taarifa za mwaka (Annual Returns), pamoja na kuimarisha usalama wa taarifa kwa kuhakikisha wanahisa na wakurugenzi wanapokea taarifa kila mabadiliko yanapofanyika ndani ya kampuni.

Regio alisema wananchi wanaotaka kutumia mfumo huo wanapaswa kuwa na Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN), namba ya simu inayotumika na anuani sahihi ya barua pepe.
Aliongeza kuwa BRELA inaendelea kutoa huduma zote muhimu katika banda la Wizara ya Viwanda na Biashara kuanzia Agosti 1 hadi 8, na kuwakaribisha wafanyabiashara,
wakulima na wananchi kutumia maonesho hayo kurasimisha shughuli zao za kiuchumi.
“Kilimo cha sasa ni kilimo biashara, hivyo ni muhimu shughuli za kiuchumi ziratibiwe na kufanyika kwa kuzingatia matakwa ya kisheria. Nanenane ni fursa nzuri kwa wananchi kupata huduma na elimu ya urasimishaji wa biashara,” alisema.
BRELA inasimamia utekelezaji wa sheria mbalimbali za urasimishaji wa biashara nchini, ikiwemo usajili wa makampuni, majina ya biashara, alama za biashara, leseni za biashara Kundi A na leseni za viwanda.


