Na Asha Mwakyonde, DODOMA
MKUU wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele, amesema jeshi hilo litaendelea kuwa karibu na wananchi kwa kutoa elimu ya kilimo bora, ufugaji wa kisasa na uvuvi wenye tija, huku likitumia maonesho ya Nanenane kama jukwaa la kuonesha mchango wake katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Amesema uwepo wa JKT katika Maonesho ya Kitaifa ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dk.John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, ni sehemu ya mkakati wa kufikisha maarifa, teknolojia na mbinu bora za uzalishaji kwa wananchi ili kuwawezesha kuongeza tija na kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza Agosti 4, 2026 na waandishi wa habari katika banda la JKT kwenye maonesho hayo, amesema ushiriki huo unalenga kuwaonesha wananchi shughuli mbalimbali zinazofanywa na JKT pamoja na fursa zinazopatikana kupitia mafunzo na uzalishaji.
Meja Jenerali Mabele, amesema banda la JKT litaendelea kuwa kituo cha kutoa elimu kwa wananchi wa Dodoma na maeneo ya jirani, ambapo wataalamu wa jeshi hilo wataendelea kutoa ushauri kuhusu kilimo bora, ufugaji na uvuvi.

“Maonesho ya Nanenane kwetu si mwisho wa utoaji wa huduma. Tutaendelea kuwepo hapa kwa lengo la kuwahudumia wananchi na kuwapa elimu kuhusu mbinu bora za uzalishaji katika sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi,” amesema.
Meja Jenerali Mabele, ameeleza kuwa JKT imekuwa ikishiriki maonesho mbalimbali nchini ikiwemo Sabasaba na Nanenane, ili kutoa fursa kwa wananchi kujionea kazi zinazotekelezwa na jeshi hilo na kujifunza teknolojia zinazoweza kuwasaidia kuongeza uzalishaji.

Aidha, ameongeza JKT inashiriki maonesho hayo katika kanda mbalimbali nchini, ikiwemo Kanda ya Mashariki na Kanda ya Ziwa, ambako wataalamu wake wanaendelea kutoa elimu kuhusu namna ya kufanya kilimo chenye tija hata katika maeneo madogo.
Amebainisha kuwa kupitia mafunzo hayo, wananchi wanaelimishwa mbinu za kisasa zinazowawezesha kuongeza uzalishaji, kuboresha ufugaji na kuendesha shughuli za uvuvi kwa ufanisi zaidi.

Akizungumzia maboresho ya maonesho hayo, Meja Jenerali Mabele, amesema JKT imekuwa ikizingatia maoni ya wananchi wanaotembelea mabanda yake kila mwaka ili kuboresha zaidi huduma na maudhui yanayooneshwa.
“Tunataka aliyekuja mwaka jana akija mwaka huu aone mabadiliko. Kama kulikuwa na mapungufu, tunayafanyia kazi ili maonesho yetu yawe bora zaidi. Ushauri wa wananchi unatupa dira ya kuboresha,” amesema.
Amesisitiza kuwa JKT itaendelea kusikiliza maoni ya Watanzania na kuyafanyia kazi ili kuhakikisha shughuli zake zinakidhi matarajio ya wananchi.
Aidha, Meja Jenerali Mabele
amewahimiza wananchi kutokuwa na hofu kutembelea maeneo yenye wanajeshi, akieleza kuwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ni jeshi la wananchi na lipo kwa ajili ya kuwahudumia.
“Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ni jeshi la wananchi. Wananchi wasiogope kututembelea, kwa sababu popote palipo na mwanajeshi yupo kwa ajili ya kusaidia pale panapohitajika,” amesema.
Amesema kupitia Nanenane wananchi wanapata nafasi ya kuona shughuli mbalimbali za JKT na kupata elimu kutoka kwa wataalamu wake kuhusu uzalishaji, mafunzo na huduma zinazochangia maendeleo ya Taifa.
JKT imewataka wananchi kutumia fursa ya maonesho hayo kutembelea banda lake ili kujifunza teknolojia na mbinu mbalimbali za kuongeza uzalishaji, kujiajiri na kuinua kipato cha familia na Taifa kwa ujumla.


