TIRA YAWAHAMASISHA WAKULIMA KUKATA BIMA KUJIKINGA NA HASARA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MAMLAKA  ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imewahamasisha wakulima na wafugaji nchini kujiunga na bima ya kilimo ili kujikinga dhidi ya hasara zinazotokana na majanga mbalimbali yanayoathiri uzalishaji, ikieleza kuwa huduma hiyo ni moja ya njia muhimu za kuongeza uhakika wa uwekezaji katika sekta ya kilimo.

Wito huo umetolewa leo Agosti 5, 2026  katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, ambako TIRA inatumia jukwaa hilo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa bima na huduma mbalimbali zinazopatikana katika sekta hiyo.

Afisa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa TIRA, Anna Massao amesema pamoja na kutoa elimu kuhusu bima ya kilimo, mamlaka hiyo pia inaeleza majukumu yake ya kusimamia sekta ya bima na kuhakikisha wananchi wanapata huduma salama na zenye kuzingatia sheria.

“Tunawakaribisha wananchi kutembelea banda letu ili wapate uelewa kuhusu bima ya kilimo na aina nyingine za bima, pamoja na kufahamu haki zao wanapotumia huduma za bima,” amesema.

Massao amesema TIRA ina jukumu la kusajili na kutoa leseni kwa watoa huduma za bima, kuandaa kanuni na miongozo ya sekta hiyo na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi viwango vinavyotakiwa.

Amesema maonesho hayo pia yanatoa fursa kwa wananchi kuwasilisha changamoto na malalamiko yanayohusu huduma za bima ili yapatiwe ufumbuzi kwa wakati.

“Tunawahimiza wananchi wenye changamoto zinazohusiana na huduma za bima kufika katika banda letu. Maafisa wetu wapo tayari kutoa ushauri na kuelekeza namna ya kutatua changamoto hizo,” amesema.

Ameongeza kuwa banda la TIRA linawakutanisha pia wadau mbalimbali wa sekta ya bima, wakiwemo kampuni za bima, wawakilishi kutoka Zanzibar na Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima, ambao wanatoa elimu na huduma kwa wananchi.

Kwa mujibu wa TIRA, ushiriki wake katika maonesho ya Nanenane unalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa bima, kukuza matumizi ya huduma hizo na kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo kwa kupunguza athari za vihatarishi vinavyoweza kusababisha hasara kwa wakulima na wafugaji.