GST YAWATAKA WACHIMBAJI KUTUMIA TAARIFA ZA KITAALAM KUEPUKA UCHIMBAJI WA KUBAHATISHA

Na Aziza Masoud, Dodoma

TAASISI ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imewataka wachimbaji wa madini na wawekezaji kutumia taarifa za kitaalamu kabla ya kuanza shughuli za uchimbaji na kusisitiza kuwa  hatua hiyo itapunguza hasara zinazotokana na uchimbaji wa kubahatisha na kuongeza tija katika sekta ya madini.

Akizungumza jana katika Maonesho ya Wakulima  Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Utawala na Uendeshaji wa GST, Neema Mhagama, alisema taasisi hiyo imejijengea uwezo mkubwa wa kitaalamu kupitia ushirikiano na taasisi mbalimbali za kimataifa, hatua iliyowezesha wataalamu wake kuwa wabobezi katika tafiti za jiolojia na uchunguzi wa madini.

Mhagama alisema jukumu la GST ni kubaini maeneo yenye uwepo wa rasilimali za madini na kutoa taarifa za kisayansi  zitakazowasaidia wachimbaji kuelekeza uwekezaji wao katika maeneo yenye fursa badala ya kutegemea kubahatisha.

“Anayetumia taarifa za kitaalamu anaongeza uwezekano wa kupata matokeo mazuri kuliko anayechimba bila kuwa na taarifa sahihi za kijiolojia,” alisema.

Alieleza kuwa ushiriki wa taasisi hiyo katika Maonesho ya Nanenane unatokana na uhusiano uliopo kati ya sekta ya madini na sekta nyingine za uzalishaji, hususan kilimo, ambapo zote zinategemea matumizi sahihi ya taarifa za kisayansi kuhusu ardhi na rasilimali zilizopo.

Mhagama alisema GST itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha taarifa za jiolojia zinawafikia wananchi kwa lengo la kuongeza tija katika uchimbaji wa madini na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.

Alisema wataalamu hao ambao wamepata mafunzo kutoka taasisi mbalimbali zikiwamo za zilizopo katika nchi  Finland na Korea Kusini, jambo lililoimarisha uwezo wa kutoa taarifa sahihi kwa wachimbaji na wawekezaji.

“Tunawakaribisha wananchi na wadau kutembelea banda letu katika Maonesho ya Nanenane na pia kufika ofisini kwetu kupata taarifa mbalimbali za jiolojia na madini. Tuna maktaba yenye taarifa nyingi zinazoweza kuwasaidia wachimbaji kufanya maamuzi sahihi kabla ya kuwekeza,” alisema.