DIB KUANZA  KUZINUSURU BENKI ZILIZO HATARINI KUFILISIKA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

BODI ya Bima ya Amana (DIB) imesema imeanza kutekeleza jukumu jipya la kusaidia benki na taasisi za fedha zinazokabiliwa na changamoto za kifedha ili zisifilisike, hatua inayolenga kulinda fedha za wateja na kudumisha utulivu wa sekta ya fedha nchini.

Akizungumza katika Maonesho ya Wakulima ya Kimataifa Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa DIB, Lwaga Mwambande, alisema taasisi hiyo sasa inaweza kuzidhamini au kuzikopesha benki zenye matatizo ya kifedha ili ziendelee kutoa huduma badala ya kusubiri zifungiwe shughuli.

Alisema hatua hiyo ni ya gharama nafuu zaidi kwa Serikali na walipakodi kuliko kusubiri benki ifilisike, hali ambayo hulazimu mfuko wa bima ya amana kutumia fedha nyingi kuwalipa wateja walioweka fedha katika benki hizo.

“Hii ni njia ya kuzuia tatizo lisikue. Tukisaidia taasisi kurejea katika hali yake ya kawaida, tunawalinda waweka amana na kuimarisha uthabiti wa mfumo wa fedha,” alisema Mwambande.

Alisema pamoja na jukumu hilo jipya, DIB inaendelea kusimamia ufilisi wa benki tisa zilizofungwa katika nyakati tofauti kwa lengo la kukusanya mali zake na kuwalipa wadai, hususan wale ambao fedha zao zinazidi kiwango kinacholindwa na bima ya amana.

Mwambande alisema kila mwananchi anayefungua akaunti katika benki yenye leseni ya Benki Kuu ya Tanzania huingia moja kwa moja kwenye mfumo wa bima ya amana bila kulipa gharama yoyote ya ziada.

Alifafanua kuwa kiwango cha juu cha fidia kinachotolewa kwa sasa ni Sh milioni 7.5 kwa kila mweka amana endapo benki itafungwa, huku wenye amana zisizozidi kiwango hicho wakilipwa fedha zao zote.

Alieleza kuwa mfuko wa bima ya amana huchangiwa na benki na taasisi za fedha zinazopokea amana kutoka kwa wananchi kwa kiwango cha asilimia 0.15 ya jumla ya amana kila mwaka, fedha ambazo huwekezwa katika maeneo salama ili kuhakikisha zinapatikana wakati wa kulipa fidia.

Aidha, aliwataka waliokuwa wateja wa Benki ya FBME na benki nyingine zilizo chini ya ufilisi kufuatilia malipo yao katika ofisi za DIB zilizopo ndani ya majengo ya Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam na Dodoma.

Alisema hadi sasa zaidi ya Sh bilioni 2.9 za fidia bado hazijachukuliwa na wateja wanaostahili, akiwataka kujitokeza ili wapate stahiki zao.