Na Aziza Masoud, Dodoma
CHUO Kikuu Cha Dodoma (UDOM) kimetengeneza mfumo wa kidijitali wa Ghala Project unaolenga kuongeza uwazi katika matumizi ya mfumo wa stakabadhi ghalani na kuwawezesha wakulima kupata taarifa za mazao yao kwa wakati.
Mfumo huo unaotekelezwa kupitia Ghala Project, unalenga kutatua changamoto zinazowakabili wakulima katika kupata taarifa baada ya kuwasilisha mazao yao maghalani, ikiwemo kutokujua hatua mbalimbali zinazofuatia hadi mazao yanapouzwa.

Mhadhiri wa Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu Angavu ya Chuo Kikuu Dodoma (UDOM), Dk. Frederick Chali, alisema utafiti uliofanywa katika sekta ya kilimo umebaini kuwa ukosefu wa uwazi wa taarifa ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili wakulima.
Alisema wakulima wengi wanapopeleka mazao yao kwenye maghala hawapati taarifa za kutosha kuhusu mwenendo wa mazao hayo, hali inayoweza kuwafanya kuwa na mashaka hata wanapopewa taarifa kuhusu hatua iliyofikiwa.

“Tumefanya utafiti kwenye eneo la kilimo na tumegundua kuna changamoto mbalimbali. Tukaangalia mfumo wa stakabadhi ghalani na changamoto zake, mojawapo ikiwa ni suala la uwazi wa taarifa kwa wakulima,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk Chali, endapo mkulima atautumia mfumo huo unampa risiti ya kidigitali mara baada ya kuwasilisha mazao yake kwenye ghala, pamoja na kumwezesha kufuatilia hatua mbalimbali za mzigo wake.

Alisema mkulima ataweza kupata taarifa kuhusu mazao yake kuanzia hatua ya kuyawasilisha ghalani hadi yanapouzwa, hivyo kuongeza uaminifu na uwazi katika mchakato mzima.
“Unapowasilisha bidhaa zako kwenye ghala, utapata taarifa ya kidijitali inayoonyesha kuwa umewasilisha bidhaa zako na utaweza kufuatilia kila hatua inayofuata hadi mzigo unapouzwa,” alisema.

Mbali na ufuatiliaji wa mazao, Dk Chali alisema mfumo huo unalenga kumsaidia mkulima kupata taarifa nyingine muhimu zinazohusiana na uzalishaji, ikiwemo upatikanaji wa mbolea na dawa za kilimo.
Alisema mkulima anapokuwa katika maandalizi ya msimu wa kilimo ataweza kupata taarifa kuhusu wanaouza mbolea na dawa, pamoja na maeneo au wakati ambao bidhaa hizo zinapatikana.
“Tunataka mkulima awe na taarifa za kutosha wakati anaandaa shamba lake. Ajue ni nani anauza mbolea na dawa, anapatikana wapi na kwa wakati gani,” alisema.
Alisema kwa sasa mfumo huo uko katika hatua ya majaribio, ambapo vyama vua msingi vitatu vilivyopo wilayani Tandahimba vimeanza kuutumia ili kubaini maeneo yanayohitaji maboresho kabla ya kuanza kutumika kwa kiwango kikubwa.
Alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha teknolojia hiyo inakidhi mahitaji halisi ya wakulima na kusaidia kuongeza uwazi katika mfumo wa stakabadhi ghalani.


