Na Aziza Masoud, DAR ES SALAAM
TANZANIA imetakiwa kutumia changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi kama fursa ya kuibua ajira, uwekezaji, ubunifu na kukuza uchumi wa kijani nchini.
Wito huo umetolewa leo Septemba 15, 2026 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yusuf Masauni, alipofungua Tanzania Green Summit 2026 yenye kaulimbiu “Turning Climate Action into Opportunity” (Kugeuza Hatua za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kuwa Fursa).
Masauni alisema mabadiliko ya tabianchi hayapaswi kuonekana kama changamoto ya mazingira pekee, bali ni suala linalogusa maendeleo ya uchumi na linaweza kutoa fursa mbalimbali kwa wananchi.

Alisema Tanzania ina nafasi kubwa ya kunufaika kupitia maeneo ya nishati safi, kilimo endelevu, utalii, usimamizi wa taka, uchumi wa buluu, teknolojia, uhifadhi wa mazingira na biashara ya kaboni.
“Hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinaweza kuwa fursa za uwekezaji, ajira, ubunifu na kukuza uchumi wa kijani,” alisema.
Alisema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa upatikanaji wa fedha za miradi ya mazingira na tabianchi, akitaja CRDB kuwa miongoni mwa taasisi zilizopata kibali chini ya Green Climate Fund (GCF).

Masauni pia alisema Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa Ofisi ya Kikanda ya Santiago Network on Loss and Damage, hatua ambayo alisema itasaidia kujenga uwezo wa nchi zinazoendelea kukabiliana na athari na hasara zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wa vijana, alisema Serikali inalenga kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kijani, akisisitiza kuwa hawapaswi kuonekana kama wanufaika wa programu za tabianchi pekee, bali wabunifu, watafiti, wajasiriamali na viongozi wa uchumi huo.
Katika eneo la biashara ya kaboni, Masauni alisema Kituo cha Rasilimali za Biashara ya Kaboni chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais kinaendelea kuwezesha utekelezaji wa miradi, huku miradi 117 ikiwa imesajiliwa na iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Alisema Serikali pia inalenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Aidha, alitaja uzalishaji wa umeme wa megawati 2,115 kupitia Mradi wa Julius Nyerere Hydropower Project (JNHPP), matumizi ya umeme katika reli ya kisasa (SGR), uendelezaji wa bandari na kuongeza matumizi ya magari ya umeme kuwa sehemu ya hatua zinazounganisha maendeleo ya uchumi na uhifadhi wa mazingira.
Masauni alisema rasilimali za madini kama nikeli, grafiti na lithiamu pia zinaweza kuiwezesha Tanzania kushiriki katika minyororo ya thamani ya teknolojia za kijani, akisisitiza umuhimu wa uongezaji thamani nchini, uhamishaji wa teknolojia na uundaji wa ajira.

Aliwataka taasisi za fedha na sekta binafsi kuongeza uwekezaji katika miradi ya uchumi wa kijani na kubuni mifumo ya kifedha itakayowezesha miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, alisema Tanzania Green Summit 2026 haipaswi kuwa jukwaa la majadiliano pekee, bali lizalishe ushirikiano, uwekezaji, teknolojia, tafiti na suluhisho zinazotekelezeka katika jamii.
Alisema Tanzania inaweza kujenga uchumi ambao ulinzi wa mazingira, ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na ustawi wa wananchi vinaenda pamoja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Grina Foundation, Redemptus Caesar, alisema taasisi hiyo imehamasishwa kuanzisha jukwaa hilo baada ya kuona namna mataifa mengine yanavyotumia fursa za mazingira kuvutia uwekezaji, mawazo mapya na ubunifu katika kujenga uchumi unaozingatia uhifadhi wa mazingira.
Caesar alisema Tanzania inahitaji kuongeza hamasa ya ndani katika kutumia fursa hizo, akieleza kuwa Grina Foundation inalenga pia kuwawezesha vijana kupitia programu mbalimbali zitakazowapa nafasi ya kuibua na kukuza mawazo yanayolenga kutatua changamoto za mazingira.

Alisema taasisi hiyo ipo tayari kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuwawezesha vijana, hususan katika ujasiriamali na ubunifu wa kimazingira, ili kuhakikisha mawazo yao yanabadilishwa kuwa fursa za kiuchumi na suluhisho zenye manufaa kwa jamii.
Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa, Suzan Ngongi, alisema Tanzania iko katika hatua muhimu ya utekelezaji wa Dira yake ya Maendeleo, hivyo kinachohitajika sasa ni kubadili mipango na mawazo mazuri kuwa uwekezaji, biashara, miundombinu, ajira na maisha bora huku mifumo ya asili ikiendelea kuwa salama na yenye tija.
Ngongi alisema changamoto kubwa iliyopo ni namna ya kuyafikisha mawazo na ubunifu wa mazingira kwenye kiwango kikubwa, akisisitiza umuhimu wa kuwaunganisha wabunifu na mitaji, masoko na sera. Alisema pia ni muhimu kuongeza idadi ya miradi inayoweza kufadhiliwa na taasisi za fedha ili Tanzania iwe na mtiririko wa miradi yenye uwezo wa kuzalisha matokeo ya kiuchumi,kimazingira na kijamii.


