SERIKALI YAPITIA SHERIA KUONDOA VIKWAZO VYA UWEKEZAJI UCHUMI WA BULUU

Na Aziza Masoud, Dar es Salaam

WIZARA ya Katiba na Sheria imesema inaendelea kupitia sheria mbalimbali zinazoweza kuwa kikwazo kwa uwekezaji na matumizi ya rasilimali za uchumi wa buluu, katika juhudi za kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kushiriki zaidi katika kukuza uchumi wa nchi.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha sheria na kanuni zinazohusu matumizi ya rasilimali zilizopo katika bahari, maziwa na maeneo mengine ya maji zinaendana na mahitaji ya uwekezaji, sambamba na kulinda maslahi ya taifa na wananchi.

Akizungumza leo, Septemba 7, 2026, jijini Dar es Salaam katika Kongamano la Tano la Kimataifa la Uchumi wa Buluu, Mkurugenzi wa Kitengo cha Uangalizi wa Utajiri Asilia na Maliasili kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Neema Mwanga, amesema serikali imeweka mkakati wa kupitia sheria zinazohusiana na sekta mbalimbali ili kuziendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema sheria ambazo zimekuwa zikikwamisha uvunaji, matumizi na uwekezaji katika utajiri asilia na maliasili zinapaswa kufanyiwa marekebisho ili kutoa nafasi kwa wawekezaji kushiriki katika kukuza uchumi wa buluu.

“Dira ya Taifa ya 2050 inahitaji sheria kuwa rafiki na wezeshi kwa uwekezaji, hivyo wizara imeweka mkakati wa kupitia sheria zinazohusiana na sekta mbalimbali na kuhakikisha zinaendana na malengo ya taifa,” amesema Mwanga.

Amesema uchumi wa buluu unatoa fursa kubwa kwa sekta binafsi, hususan katika shughuli za uvuvi wa baharini, uzalishaji na uchangaji wa mwani pamoja na uzalishaji wa bidhaa zinazotokana na rasilimali za bahari.

Kwa mujibu wa Mwanga, uwepo wa mazingira mazuri ya kisheria utampa mwekezaji uhakika wa taratibu na kanuni za kufuata, huku serikali ikihakikisha uwekezaji huo unaleta manufaa kwa wananchi na kuchangia maendeleo endelevu.

Amesema pamoja na kuvutia uwekezaji, wizara inaendelea kuweka uwiano kati ya uwekezaji na jukumu la kulinda utajiri asilia na maliasili za nchi ili rasilimali hizo zitumike kwa tija kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha, amesema wananchi wanapaswa kushirikishwa na kupewa uelewa kuhusu fursa zinazopatikana katika uchumi wa buluu ili waweze kushiriki moja kwa moja katika kunufaika na rasilimali hizo.

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Daniel Mbaki, amesema kuwepo kwa mfumo madhubuti wa utatuzi wa migogoro ni sehemu muhimu ya kujenga mazingira bora ya uwekezaji katika uchumi wa buluu.

Amesema matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro, ikiwemo upatanishi na usuluhishi, yanapaswa kupewa kipaumbele ili migogoro inayoweza kujitokeza kati ya wawekezaji na wadau wengine ipatiwe ufumbuzi kwa haraka na kwa njia stahiki.

Mbaki amesema kitengo cha utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala kimesajili wataalamu wanaotoa huduma za upatanishi, usuluhishi na uwezeshaji wa majadiliano, huku akiwakaribisha wataalamu wengine kujisajili kupitia mfumo wa NARIS.

Hatua ya kupitia sheria na kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro inatarajiwa kuongeza uhakika kwa wawekezaji na kufungua zaidi fursa za sekta binafsi kushiriki katika uchumi wa buluu, ambao umetajwa kuwa miongoni mwa maeneo muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.