SERIKALI YASISITIZA SAYANSI,TAFITI KUWA KICHOCHEO CHA UCHUMI WA BULUU

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

SERIKALI imesisitiza umuhimu wa kuimarisha sayansi, tafiti na matumizi ya teknolojia katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa buluu, ikisema Tanzania ina rasilimali nyingi za bahari, maziwa, mito na maeneo ya pwani ambazo bado hazijatumika kikamilifu.

Hayo yameelezwa katika Kongamano la Tano la Kimataifa la Sayansi na Uchumi wa Buluu, lililoandaliwa na Chuo Cha Bahari Dar es Salaam (DMI) ambapo serikali imesema mafanikio ya sekta hiyo yatategemea zaidi upatikanaji wa tafiti zenye kutoa majibu ya changamoto zilizopo na kubadili matokeo ya kisayansi kuwa fursa za kiuchumi.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Makamu wa Rais Deogratus Ndejembi,Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira,Mhandisi Hamad Masauni alisema Tanzania inahitaji tafiti zitakazosaidia kufahamu uwezo halisi wa rasilimali za majini, kuboresha uzalishaji, kutengeneza teknolojia mpya, kuongeza thamani ya bidhaa na kulinda mazingira.

“Uchumi wa buluu wa kisasa unahitaji wataalamu wenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kutumia teknolojia mpya. Taasisi za elimu ya juu na utafiti zina nafasi kubwa katika kuzalisha rasilimali watu wenye uwezo wa kuendesha mageuzi ya sekta hii,” alisema.

Alisema rasilimali za bahari, maziwa, mito, maeneo ya pwani na mazingira mengine ya majini zina nafasi muhimu katika kuongeza uzalishaji wa chakula, biashara, uwekezaji, ajira na ustawi wa jamii.

Alisema, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeitambua uchumi wa buluu kuwa miongoni mwa sekta za kimkakati zitakazochochea uchumi shindani, jumuishi na endelevu.

“Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kukuza sekta hiyo, ikiwamo kuimarisha uratibu wa masuala ya uchumi wa buluu, kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi na ufugaji wa samaki katika uchumi na kukuza biashara na uwekezaji unaotokana na rasilimali za majini,”alisema Masauni.

Alisema taasisi za utafiti na elimu ya juu zinatakiwa kuelekeza nguvu katika tafiti zitakazotoa suluhisho la changamoto za maendeleo badala ya matokeo kubaki katika machapisho na makaratasi.

Pia iliwataka wawekezaji wa sekta binafsi kutumia fursa zinazopatikana katika uchumi wa buluu, zikiwamo teknolojia za baharini, kuongeza thamani ya mazao ya bahari, biashara ya kaboni buluu na huduma za kidijitali.

Alisema, serikali ilisisitiza kuwa hakuna nchi inayoweza kufanikisha kikamilifu maendeleo ya uchumi wa buluu peke yake kutokana na bahari na rasilimali za majini kuunganisha mataifa mbalimbali.

Masauni ametoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika tafiti za kisayansi, matumizi ya teknolojia, uendelezaji wa wataalamu, usimamizi wa rasilimali za pamoja na uhifadhi wa mazingira.

“Tunatarajia kongamano hili litatoa mapendekezo yanayotekelezeka yatakayoboresha sera, kuimarisha mazingira ya uwekezaji, kuongeza matumizi ya teknolojia na kuhakikisha rasilimali za majini zinatumika kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema Masauni.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile alisema serikali imejipanga kuelekea kwenye utekelezaji kwa dira ya 2050 kuhakikisha inanufaika na uchumi wa buluu.

Alisema katika sekta hiyo rasilimali watu ni muhimu pamoja na maelezo ya teknolojia na hivyo inahitajika inahitaji mtaalamu mwenye maarifa ujuzi uwezo wa kutumia hizo kwa nini taasisi zetu za elimu na utafiti na wajibu wa kuendelea kuandaa wataalamu wanaokidhi mahitaji ya sasa na baadae.

“Katika eneo hili Chuo Cha Bahari Dar es Salaam na viongozi wengine wana nafasi muhimu katika kuunganisha elimu utafiti ubunifu na mahitaji ya sekta hii,naomba kutumia nafasi hii kupongeza ubunifu huu kwa kiwango cha juu kabisa cha chuo chetu cha mwanzo kuamua kuanzisha jukwaa hili muhimu niliwakutanisha watawa wa ndani na nje ya nchi yetu ili kuchakata vyema namna ambavyo.

“Tunaweza kunufaika na uchumi wa bluu ikiwa ni eneo muhimu kuelekea kwenye mradi wa dira 2050 hongereni sana DMI hongera sana mwenyekiti wa bodi hongera sana mkuu wa chuo na timu nzima mheshimiwa maeneo yanayojadiliwa katika mkutano huu yanaendana na mwelekeo wa dira 2050 inayosisitiza ujenzi wa uchumi wenye ushindani unaotegemea teknolojia na ubunifu,”alisema Kihenzile.

“Pamoja na matengenezo rasilimali watu wa taifa kwa upande wa uchukuzi dira hii inatupa wajibu wa kuendelea kuimarisha mifumo ya uchukuzi ili kuwezesha Tanzania kutumia vyema nafasi kubwa pia kuimarisha biashara ya ndani na kimataifa na hivyo kuongeza ushindani,”alisema Kihenzile.

Kongamano hilo limewakutanisha watafiti, watunga sera, sekta binafsi, taasisi za elimu ya juu, wabunifu na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania kujadili namna ya kutumia sayansi na teknolojia kuharakisha maendeleo ya uchumi wa buluu.