BRELA:USIPOSAJILI NEMBO, MWINGINE ANAWEZA KUICHUKUA

Na Mwandishi Wetu,Geita

WAFANYABIASHARA wanaotumia majina na alama za biashara bila kuzisajili wameonywa kuwa wanaweza kuingia katika migogoro ya umiliki endapo mtu mwingine atatangulia kuzisajili.

Onyo hilo limetolewa na Afisa Usajili wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Athumani Makuka, wakati akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda la taasisi hiyo katika Maonesho ya Tisa ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.

Makuka amesema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakitumia nembo na alama za biashara kwa muda mrefu bila kuzisajili, hali inayoweza kusababisha matatizo pale mtu mwingine anapochukua hatua za kuzisajili.

“Tunawasistiza wafanyabiashara waje kusajili alama zao kwa sababu kuna kesi ambazo zimejitokeza. Mtu anakuwa na nembo hajaisajili, baadaye mtu mwingine anakuja kuisajili na ndipo mgogoro unaanza,” amesema.

Amesema BRELA inatoa huduma za usajili wa majina ya biashara, kampuni na alama za biashara, pamoja na elimu kuhusu namna ya kulinda ubunifu na uvumbuzi wa wananchi.

Kwa mujibu wa Makuka, BRELA pia imekuwa ikitoa elimu kwa wabunifu na wavumbuzi kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kulinda kazi zao dhidi ya matumizi yasiyoruhusiwa.

Amesema katika maonesho hayo, taasisi hiyo imepokea pia mvumbuzi kutoka Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), aliyefika kupata maelekezo kuhusu namna ya kusajili na kulinda uvumbuzi wake.

“Tumepokea mvumbuzi mmoja kutoka VETA ambaye amekuja kuulizia namna ya kusajili uvumbuzi wake. Hatuwezi kueleza kwa undani uvumbuzi huo kwa sababu bado haujakamilika, lakini tumempa elimu kuhusu hatua zinazohitajika ili uweze kulindwa,” amesema.

Katika hatua nyingine, Makuka amesema BRELA imeboresha mfumo wake wa kidijitali wa BRELA Online System (BOS), unaolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za usajili kwa wananchi.

Amesema mfumo huo ulioboreshwa unamwezesha mtumiaji kutumia namba moja ya NIDA na akaunti moja kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na BRELA.

Kwa upande wake, Mhandisi kutoka VETA, Audiface Tarimo, amesema amefika katika banda la BRELA baada ya kukumbana na changamoto kuhusu jina la biashara alilolisajili mwaka 2022.

Tarimo amesema alihitaji kubadilisha usajili wa jina hilo ili aweze kulisajili kama kampuni, hatua ambayo amesema amepewa msaada na maafisa wa BRELA.

“Nilisajili jina la biashara mwaka 2022, sasa nilihitaji lile jina la biashara kulisajili kama kampuni. Nimefika hapa na nimepata msaada wa kuweza kuhuisha lile jina ili mwisho wa siku niweze kusajili kampuni,” amesema.

Amesema ameridhishwa na huduma aliyopata na kuwataka Watanzania wenye changamoto kuhusu huduma za BRELA kufika katika banda hilo kwa ajili ya kupata elimu na msaada