TOTAL ENERGIES YAFUNGUA FURSA ZA AJIRA, BIASHARA DODOMA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

UWEKEZAJI wa kampuni ya Total Energies nchini umeendelea kufungua fursa za ajira na biashara kwa wananchi, huku uzinduzi wa kituo kipya cha kampuni hiyo eneo la Vikonje, nje kidogo ya Jiji la Dodoma, ukitajwa kuwa kichocheo cha shughuli za kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo.

Kituo hicho kipya kimefungua ajira kwa vijana 12, huku uwepo wake ukitarajiwa kuongeza fursa nyingine za biashara kwa wananchi wanaokizunguka na kuchochea mzunguko wa fedha katika uchumi wa eneo hilo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo hicho jana, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alisema uwekezaji wa kampuni hiyo una umuhimu kwa mkoa kutokana na fursa zinazotokana na kila kituo kipya kinachofunguliwa.

Alisema uwekezaji huo si suala la kuongeza huduma za nishati pekee, bali pia una mchango katika kukuza uchumi wa wananchi kupitia ajira na shughuli mbalimbali za kibiashara zinazochipuka katika maeneo yanapowekwa vituo hivyo.

“Uwekezaji wa Total Energies kwa Mkoa wa Dodoma una maana sana kwa sababu kila kituo kipya kinachofunguliwa kinaongeza fursa ya ajira kwa wananchi, hususani vijana,” alisema Senyamule.

Aidha, Senyamule aliitaka kampuni hiyo pamoja na taasisi nyingine za umma na binafsi kuhakikisha huduma wanazozitoa kwa wananchi zinaendelea kuwa bora na endelevu.

Alisema Wiki ya Huduma kwa Wateja inapaswa kutumika kama fursa ya taasisi kujitathmini, kusikiliza changamoto na ushauri wa wateja na kuchukua hatua za kuboresha huduma.

“Nitumie nafasi hii kutoa wito kwa taasisi zote za Serikali na sekta binafsi kuitumia wiki hii kama wiki ya kuendelea kuwafanya wateja watufahamu, lakini tuwape huduma bora na endelevu, tuchukue changamoto zao na ushauri ili kuendelea kuimarisha huduma tunazowapa, maana bila wao sisi hatuna kazi za kufanya,” alisema.

Senyamule pia aliipongeza Total Energies kwa kuendelea kuwekeza nchini kwa takribani miaka 57, akisema uwekezaji wake katika miundombinu ya nishati una mchango katika shughuli za kiuchumi na maendeleo ya nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa kituo hicho, Edwin Sanga, alisema tangu kituo hicho kuanza kutoa huduma kimepokea idadi kubwa ya wateja, hali ambayo amesema imezidi matarajio yao.

Sanga alisema mafanikio hayo yanawapa motisha ya kuendelea kuboresha huduma na kuhakikisha kila mteja anayefika kituoni hapo anapata huduma inayokidhi mahitaji yake.

“Tangu tumefungua kituo hiki tumepata matokeo mazuri ya wateja, wamekuja kwa wingi, tunawashukuru sana wakazi wa Dodoma. Tunafahamu imani ya wateja hujengwa kila siku kupitia huduma bora, ubora wa bidhaa na uzoefu mzuri, hivyo ahadi yetu ni kuendelea kuwahudumia kwa viwango vya hali ya juu,” alisema.

Uzinduzi huo uliwashirikisha viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mkoa wa Dodoma, wadau wa biashara pamoja na maofisa wa Total Energies, akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa vituo vya kampuni hiyo, Abdulrahman Sadik.