MAKAMU WA RAIS ATEMBELEA BANDA LA TANESCO KATIKA HAFLA YA UTIAJI SAINI LESENI ZA UTAFUTAJI WA MAFUTA NA GESI

📌Aelezwa jinsi TANESCO inavyozalisha Umeme kupitia Vyanzo mbalimbali vya nishati ikiwemo gesi asilia.

Na. Mwandishi wetu, Dar Es Salaam.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ametembelea leo banda la Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika hafla ya utiaji Saini Leseni za Utafutaji wa Mafuta na Gesi katika vitalu vya Mnazi Bay North, West Songo Songo, Eyasi Wembere na Lindi-Mtwara, iliyofanyika katika ukumbi and wa Julius Nyerere International Convention Center (JNICC) ambapo amepokea maelezo kuhusu juhudi za Shirika katika kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa kutosha na wa uhakika nchini.

Akiwa katika banda hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amemweleza Makamu wa Rais namna Shirika linavyotumia vyanzo mseto vya Nishati katika uzalishaji wa umeme, ikiwemo gesi asilia, ili kuimarisha uzalishaji na kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme kwa wananchi.

Katika maelezo hayo, Bw. Twange amebainisha kuwa TANESCO inazalisha umeme kupitia vituo mbalimbali vinavyotumia gesi asilia, vikiwemo Kinyerezi I na II, Ubungo I, II na III, Tegeta pamoja na Mtwara I na II.

Juhudi hizo ni sehemu ya mikakati ya kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya nishati, hatua inayolenga kusaidia kukidhi mahitaji ya umeme yanayoongezeka na kuimarisha upatikanaji wake kwa matumizi ya majumbani, biashara na shughuli za uzalishaji.