MRADI WA LNG LINDI MBIONI KUANZA, NI MRADI WENYE THAMANI KUBWA KUSINI MWA AFRIKA-NDEJEMBI

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema Tanzania ipo hatua za mwisho za maandalizi ya kuanza kutekeleza mradi mkubwa wa kuchakata na kusafirisha gesi asilia kwa njia ya kimiminika (LNG) mkoani Lindi, akieleza kuwa mradi huo ni wa kimkakati kwa uchumi wa taifa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Oktoba 28, 2026, wakati wa hafla ya utiaji saini leseni za utafutaji wa mafuta na gesi asilia, Ndejembi amesema Serikali ya Tanzania imekamilisha maandalizi yake na inawasubiri wabia wa kimataifa kukamilisha taratibu zilizobaki ili mradi huo uanze kutekelezwa.

Amesisitiza kuwa mradi huo una umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya taifa, akibainisha kuwa una matarajio ya kuongeza uwekezaji, kuchochea shughuli za kiuchumi na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika sekta ya mafuta na gesi asilia.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya utafutaji na uendelezaji wa gesi asilia kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na wadau wengine, huku ikihakikisha rasilimali hizo zinasimamiwa kwa kuzingatia maslahi ya taifa.

Katika hatua nyingine, Ndejembi ametoa wito kwa wadau wote wa sekta hiyo kushirikiana kwa uadilifu, uwajibikaji na uzalendo ili kuhakikisha uwekezaji wa mafuta na gesi unachangia maendeleo endelevu na ustawi wa Watanzania.