WAFANYABIASHARA KARIAKOO WAILILIA BoT MAKATO YA MIAMALA

Na Aziza Masoud, Dar es Salaam

WAFANYABIASHARA wa Kariakoo wameiomba Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuangalia upya gharama za miamala ya kielektroniki ili kuwavutia wafanyabiashara wengi zaidi kuachana na matumizi ya fedha taslimu.

Wamesema licha ya kutambua umuhimu wa malipo ya kidijitali katika kurahisisha biashara, gharama za miamala zinazotozwa zinaweza kuwa kikwazo kwa matumizi mapana ya mifumo hiyo.

Kauli hiyo imekuja wakati BoT ikiimarisha kampeni ya kuhamasisha matumizi ya mifumo rasmi ya malipo ya kielektroniki, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupunguza utegemezi wa fedha taslimu na kujenga uchumi wa kisasa.

Akizungumza Novemba 11, 2026, jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Donath Kibwana, amesema ni muhimu mifumo hiyo iwe na gharama nafuu ili wafanyabiashara waone manufaa ya kuitumia.

Amesema wafanyabiashara wanatambua kuwa malipo ya kidijitali yanaokoa muda, kwa kuwawezesha kupokea fedha papo hapo bila kulazimika kwenda benki kusubiri huduma za fedha taslimu.

Hata hivyo, amesema makato yanayotozwa yanapaswa kuangaliwa upya kwa kuzingatia viwango vinavyotumika katika nchi nyingine.

Ametolea mfano Kenya, ambako matumizi ya fedha taslimu yamepungua kutokana na kuimarika kwa mifumo ya malipo ya kielektroniki, akisema Tanzania inahitaji kuweka mazingira yatakayowavutia wafanyabiashara kutumia huduma hizo.

Wakati wafanyabiashara wakitoa maoni hayo, BoT imesema inaendelea na juhudi za kuhamasisha matumizi ya mifumo rasmi ya malipo ya kidijitali ili kupunguza changamoto zinazotokana na utegemezi wa fedha taslimu.

Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa wa BoT, Lucy Shaidi, amesema lengo la mkutano huo na wafanyabiashara wa Kariakoo ni kuwaelimisha kuhusu mifumo iliyopo, faida zake na namna ya kuitumia kwa usalama.

Amesema pia mkutano huo umelenga kuipa BoT fursa ya kusikiliza changamoto zinazowakabili wafanyabiashara na kupata maoni yatakayosaidia kuboresha huduma za malipo nchini.

Shaidi amesema matumizi ya mifumo ya kidijitali yanaweza kusaidia kulinda mitaji ya wafanyabiashara kwa kupunguza hatari za wizi, kupokea noti bandia na changamoto za kubeba fedha nyingi taslimu.

Ameongeza kuwa kila muamala wa kielektroniki huacha kumbukumbu zinazomwezesha mfanyabiashara kufuatilia mauzo, kutathmini mwenendo wa biashara na kupunguza migogoro ya kifedha.

Kwa mujibu wake, kumbukumbu hizo zinaweza pia kuwawezesha wafanyabiashara kupata fursa za mikopo kutoka taasisi za fedha kwa kuwa zinaonesha mwenendo halisi wa shughuli zao.

Amezitaja baadhi ya njia za malipo ya kidijitali kuwa ni kadi za benki, mashine za malipo (POS), simu za kiganjani, huduma za benki mtandao, lipa namba na misimbo milia (QR Code).

Amesema BoT imejenga na kusimamia miundombinu ya malipo ya kidijitali, ikiwemo Mfumo wa Malipo ya Papo Hapo Tanzania (TIPS), unaowezesha kufanya malipo kupitia lipa namba na QR Code.

Aidha, amesema benki hiyo inaendelea kutoa leseni na kusimamia watoa huduma za fedha pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi salama ya mifumo hiyo.

Shaidi amesisitiza kuwa uchumi wenye matumizi madogo ya fedha taslimu haumaanishi kuondoa kabisa fedha hizo, bali kupunguza utegemezi wake kwa kuhamasisha matumizi ya mifumo rasmi ya malipo.

Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi imara, wa kisasa na wa kipato cha juu kupitia matumizi ya teknolojia na uchumi wa kidijitali.

Kwa upande wake, Kibwana ameomba BoT kuendeleza vikao vya majadiliano na wafanyabiashara ili kutatua changamoto zinazojitokeza na kuhakikisha mifumo ya malipo ya kielektroniki inakuwa rafiki kwa watumiaji.