Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kupitia operesheni maalum kwa mwaka 2024 imekamata kilogramu 2,327,983.66 za dawa za kulevya ikiwemo kg 448.3 zilizokuwa zimefichwa ndani ya Jahazi lililosajiliwa nchini Pakstani kwa namba B.F.D 16548.
Akizungumza jana Januari 9,2025 Kamisha Mkuu wa DCEA,Kamishna Jenerali Aretas Lyimo amesema
mwishoni mwa mwaka 2024,DCEA kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ilikamata kilogramu 673.2 za Methamphetamine na heroin.
“Kwa mwaka 2024, jumla ya kilogramu 2,327,983.66 za dawa za kulevya zilikamatwa,hiki ni kiasi kikubwa cha dawa za kulevya kuwahi kukamatwa nchini na endapo kiasi hiki kingefanikiwa kusambazwa kingeleta athari kubwa na kurudisha nyuma ustawi wa Taifa letu.

“DCEA ilikamata kilogramu 673.2 za Methamphetamine na heroin,kati ya dawa hizo, kilogramu 448.3 zilizowahusisha raia nane (8) wa Pakistani zilikamatwa Bahari ya Hindi zikiwa zimefichwa ndani ya jahazi lililosajiliwa nchini Pakstani kwa namba B.F.D 16548, aidha, kilogramu 224.9 zilikamatwa kwenye fukwe za Bahari ya Hindi mkoani Dar es Salaam,”amesema Kamshina Lyimo.
Amesema katika dawa hizo zilizokamatwa mwaka jana zimo pia kilogramu 673.2 za Methamphetamine na heroin.

Amesema mbali na heroin DCEA pia ilikamata bangi Kwa wingi zaidi Kwa mwaka jana ikifuatiwa na methamphetamine, heroin na dawa tiba yenye asili ya kulevya aina ya Fentanyl.
“Aidha kwa mara ya kwanza dawa mpya ya kulevya aina ya 3-4 Methylene-Dioxy-Pyrovalerone (MDVP) ilikamatwa nchini. Ufanisi huu umetokana na operesheni zilizofanyika katika maeneo mbalimbali ndani ya nchi yetu ikiwemo eneo la Bahari ya Hindi ambapo dawa za kulevya zimekuwa zikiingizwa kwa kiasi kikubwa nchini kupitia majahazi,”amesema Kamishna Lyimo.

Katika hatua nyingine Kamishna Lyimo amesema serikali imeendelea kuweka mkazo katika kuhakikisha inaikinga jamii dhidi ya madhara yatokanayo na matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
“Kwa mwaka 2024, takribani watu milioni 28 walipewa elimu kuhusu tatizo la dawa za kulevya kupitia nyanja mbalimbali za uelimishaji, zikiwemo vyombo vya habari, semina na warsha, matamasha, mikusanyiko mbalimbali, na matukio ya kitaifa.

“Katika juhudi za kupanua huduma za tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya nchini, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, imeongeza vituo viwili vya matibabu (MAT Clinics) katika mikoa ya Pwani na Tanga, na hivyo kufanikisha kuwa na jumla ya vituo 18 vya MAT nchini. Vituo hivi vimesajili na vinawahudumia jumla ya waraibu 18,170,”amesema Kamishna Lyimo.
Amesema vituo hivi vinatoa huduma za utengamao kwa waraibu wa dawa za kulevya aina ya afyuni kama vile heroin na baadhi ya dawa tiba zenye asili ya kulevya kama vile Tramadol na Pethidine.

Ameongeza kuwa DCEA imeongezeka nyumba sita (06) za upataji nafuu (Sober house) na hivyo, kufikia nyumba 62 ambapo jumla ya waraibu 17,230 walipata huduma za utengamao.
