RAIS DK.SAMIA KUFUNGUA SOKO LA KARIAKOO

Na Aziza Masoud,Dar es salaam

RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara mkoani Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine atafungua soko kuu la Kimataifa la Kariakoo ambalo ujenzi wake umekamilika mwishoni mwa mwaka jana.

Kufuatia ufunguzi huo wafanyabiashara wa biashara ndogondogo  waliopo katika soko hilo ambao wamefunga njia zakuingilia  kwenye  soko wametakiwa kuondoka ili kuwaachia waliochukua vizimba kufanya biashara kwa uhuru.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila alisema kuwa ziara hiyo ya Rais Dk. Samia inatarajiwa kufanyika Februari nane mwaka huu ambapo amewataka wananchi kujitokeza kwa ajili ya kumsikiliza kwakuwa atazungumza nao wakati akifungua soko hilo.

“Ujio wa rais Dk. Samia mkoani  kwetu ( Dar es Salaam) umetupa heshima na hii ni mara ya kwanza tangu aapishwe kuwa rais,Dk.Samia ametupa heshima kubwa kwakuwafanya ziara,tunamtarajia atuzindulie soko kuu la Karikakoo Februari  nane  kuanzia saa mbili asubuhi hivyo nawaomba wananchi tujitokeze,”alisema Chalamila.

Alisema soko la Kariakoo lilipoungua rais Dk.Samia alitoa maelekezo yakuhakikisha linajengwa upya kwa ajili yakuwasaidia wafanyabiashara kupata sehemu  yakufanyia biashara.

Alisema pamoja na kutoa maelekezo Rais Dk.Samia alipeleka Sh Bilioni 28 kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo ambalo lipo chini ya  Shirika la Masoko Kariakoo.

“Shirika la Masoko Kariakoo wamejitahidi kuhakikisha wafanyabiashara wote wanarudishwa katika soko jipya na la zamani,wafanyabiashara wote waliopata mikataba wanafahamu hatua zote walizopitia mpaka kupata vizimba,”alisema Chalamila.

Alisema maboresho ya soko hilo yameongeza tija  kubwa na kwamba kwa sasa soko lina vizimba zaidi ya 1500 ambavyo vinatarajia kuingiza wafanyabiashara zaidia ya 1000,eneo la kuegesha magari ambalo lina uwezo wakuegesha gari zaidi ya 400,magodauni ya kisasa pamoja na maeneo mawili ya chini.

Alisema wakati uzinduzi huo ukikaribia wafanyabiashara ndogondogo wanaofanya biashara katika njia zakuingilia katika soko hilo wanatakiwa kuondoka katika maeneo hayo.

“Wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika njia zakuingilia sokoni watoke mara moja,waziache wazi njia hizo  ili kusaidia waliochukua vizimba wakae na kufanya biashara kwa uhuru,waliofunga barabara nawaambia sio wakati wakutumia nguvu huu,soko la Kariakoo ni muhimu na linategemewa na kutarajiwa kuendelea kuwa kielelezo kikubwa katika diplomasia ya uchumi ha mambo ya biashara,”alisema Chalamila.