Na Hafidh Kido,Dar es Salaam
WAKATI nchi za Afrika zikiendelea kuwa mwathirika mkubwa wa athari za mabadiliko ya Tabianchi, wadau wa mazingira wameona haja ya kuhusisha wanahabari katika mapambano hayo.
Katika mafunzo yaliyotolewa jana kwa njia ya mtandao na Media for Environment, Science, Health and Agriculture (MESHA) kupitia programu ya Cross Boarder Science Café imewazindua wanahabari juu ya kutazama upya hali ya mabadiliko ya tabianchi, usawa wa kijinsia, afya na habari zitakazoleta mabadiliko chanya.

Aidha, mtandao huo umeunganisha wanahabari kutoka nchi sita za Afrika ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Zimbabwe, Zambia na Malawi ambapo kwa pamoja wamekubaliana kuongeza nguvu katika uchunguzi wa kina juu ya Habari za mabadiliko ya tabianchi.
Mwakilishi wa kimataifa kutoka ActionAid International, Teresa Anderson, amesema ipo haja ya kuweka usawa wakati wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Kwa sababu mataifa mengi yanayoathirika kwa kiasi kikubwa yana mvhango mdogo katika kuharibu mazingira. Nchi Tajiri zinachafua mazingira kwa wingi, wanahitajika kuchukua hatua za haraka kupunguza uchafuzi wa gesi joto lakini kutoa fedha za kusaidia kuabiliana na Athari za mazingira,” alisema Teresa.
Alibainisha kuwa uandishi wa tabianchi lazima uweke mbele haki za jamii zinazoathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake kiongozi wa Mkakati na Masuala ya Kiufundi, African Centre for Health, Climate and Gender Justice Alliance (ACHCGA), Imali Ngusale amesema kuchagua kushirikiana na vyombo vya habari kutasaidia kuleta matokeo ya haraka.
“Wataalamu watawapa taarifa za kisayansi wanahabari kwa ajili ya kuripoti hali halisi, vyombo vya habari vina jukumu la kufuatilia utekelezaji wa ahadi za wakuu wan chi walizotoa kwenye mikutano ya COP kuhusu tabianchi,” alisema Imali.
Violet Otindo, amezungumzia juu ya masuala ya kiafya na jinsia yanavyoingiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, alibainisha kuwa upungufu wa mvua husababisha uhaba wa maji, upungufu wa chakula unaosababisha pia matatizo ya kiafya.
“Wanawake katika familia za kiafrika ndio wanaofanya kazi nyingi, athari za kimazingira huwakumba zaidi na hasa ukatili wa kijinsia kutoka kwa wenza wao,” alisema Otindo.


