DCEA YAKAMATA KILOGRAMU 299.8 ZA MIRUNGI

Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama hususan Jeshi la Polisi, kuanzia Februari  10 hadi 16,  2026, imefanya operesheni maalum katika vijiji vya Marieni na Mhero vilivyopo kata ya Chome, wilaya ya Same, Kilimanjaro na kukamata kilogramu 299.8 .

Akizungumza mara baada ya operesheni hiyo, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo alisema katika operesheni hiyo DCEA, ilikamata  kilogramu 299.8 za dawa za kulevya aina ya mirungi pamoja na kuteketeza ekari 203 za mashamba ya mirungi ambapo watu saba walikamatwa kuhusiana na uhalifu huo.Aliongeza kuwa, licha ya jitihada za muda mrefu za utoaji elimu na operesheni za mara kwa mara, bado kuna watu wachache wanaoendelea kukaidi sheria za nchi.

“Serikali imefikisha huduma muhimu ikiwemo umeme na maji safi pamoja na miradi ya kilimo na ufugaji.

“Wananchi wengi wameanza kujishughulisha na mazao mbadala kama vile vitunguu, viazi, kabeji, parachichi na kahawa,” amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Vilevile, amesisitiza kuwa, Mamlaka itaendelea kushirikiana na viongozi wa vijiji, kata, wilaya na mkoa pamoja na wadau wengine kutoa elimu na kutekeleza operesheni endelevu.Lengo ni kuhakikisha tatizo la mirungi linadhibitiwa kikamilifu katika mkoa wa Kilimanjaro.

Kwa upande wake Mtendaji wa Kijiji cha Mhero, Hamad Waziri Hamad amesema operesheni hiyo itakuwa msaada mkubwa katika kijiji hicho kwa sababu itasaidia vijana wengi kuachana na kilimo na matumizi ya mirungi.

Amesema, katika kilimo cha mirungii madhara yalikuwa mengi kwa vijana ikiwemo vitendo vya uhalifu na kuhatarisha usalama wa wakazi wa maeneo hayo.

Nao baadhi ya wakazi wa Chome akiwemo, Rafael Kisenge mkulima wa mazao mseto wamethibitisha uwepo wa fursa zilizopo katika maeneo hao ikiwemo ardhi yenye rutuba inayostawisha mazao halali.“Naishukuru serikali kwa kuweka mfumo mzuri, tunapata ruzuku ya pembejeo na hata tukilima katika eneo dogo tumekuwa tukipata faida. Hivyo hakuna sababu za kufanya kilimo haramu, ” amesema Kisenge.

Kadhalika, Mohamed Athuman Mbwabo mkazi na dereva wa maroli amesema, kufuatia operesheni zilizofanyika baadhi ya wakazi wa maeneo hayo wameachana na kilimo cha mirungi na wachache waliokaidi, wamekamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inatoa wito kwa wananchi kuendelea kushiriki katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

l