TRA YAFUNGUA KITUO KIPYA CHA HUDUMA ZA KODI MASAKI DSM

MWENDA AONYA WANAODANGANYA KUWA NA UWEZO KUFUTA MADENI YA KODI
TRA YAJIVUNIA MFUMO WA IDRAS, KUENDELEA KUTOA ELIMU

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imefungua kituo kipya cha huduma katika eneo la Masaki Dar es Salaam ambacho kipo chini ya mkoa kodi Kinondoni lengo likiwa ni kuendelea kusogesa huduma kwa wananchi na kurahisisha ulipaji wa kodi.

Akizindua kituo hicho Februari 17,2026 Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema kufunguliwa kwa kituo hicho kunatokana na masaki kuwa eneo la kimkakati la biashara hivyo kitawawezesha watu wote wanaostahili kulipa kodi katika eneo hilo kulipa kodi wanazostahili.

Amesema kufunguliwa kwa kituo hicho pia ni miongoni mwa mikakati ya TRA ya kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza wigo wa kodi hali ambayo inaweza kupunguza viwango vya kodi katika siku za usoni iwapo kutakuwa na idadi kubwa ya walipakodi.

“Sisi tunayo dhamira ya kuona viwango vya kodi vinapungua lakini haviwezi kupungua bila kuongeza wigo wa kodi, hivyo tunapaswa kuhakikisha kila anayestahili kulipa kodi analipa kulingana na kipato chake kwa mujibu wa sheria” amesema Mwenda.

Amesema kwa kuzinduliwa kituo hicho kilanayestahili kulipa kodi atalipa na kutakuwa na huduma bora kwa walipkodi wote huku akisisitiza kufunguliwa kwa vituo vya kodi vya kimkakati kwenye maeneo yenye mzunguko mkubwa wa biashara kwenye mikoa yote.

Aidha Kamishna Mkuu Mwenda amewataka wafanyabiashara wenye madeni ya kodi kufika kwenye ofisi za mamlaka hiyo kutafuta suluhu badala ya kuhangaika na madalali mitaani.

Amesema kuna madalali wamekuwa wakiwadanganya wafanyabiashara kuwa wanauwezo wa kuwafutia madeni yao jambo ambalo haliwezekani.

Kamishna Mwenda amesema kwa kawaida deni la kodi halifutiki mpaka mhusika anapoamua kulilipa au kulipinga na kushinda kesi mahakamani.

Alisema kuna baadhi ya wafanyabiashara wenye madeni ambao wanadhani kuwa wanaweza kufanya mchezo kwa kuwatumia watu wa mitaani na madeni yakafutika hali aliyoielezea kuwa ni kujidanganya na kupoteza muda wao.

“Nataka niwaambie wafanyabiashara tena wa nchi nzima kuwa kodi haifutiki isipokuwa kwa mambo mawili tu, aidha umeilipa au umeipinga ukaenda mahakamani na mahakama ikasema vinginevyo lakini nje ya hapo utadanganywa tukikugundua utalipa gharama mara mbili utalipa kodi yenyewe na faini,” alisema

Alisema mfanyabiashara yeyote mwenye changamoto ya kikodi anapaswwa kufika kwenye mamlaka hiyo kupata ushauri kwa wahusika badala ya kuhangaika na watu wa mitaani wasiokuwa na ujuzi wa kodi.

Alisema wafanyabiashara pia wanaweza kuwatumia washauri wa kodi ambao wamesajiliwa kisheria kufanya kazi hiyo badala ya kutafuta njia za mkato mkato kwa watu wa mitaani.

“Unaweza kupata ugonjwa wa moyo kwa kudanganywa, ukiwa na deni la kodi dawa ni moja tu kulilipa kwa wakati na kwa usahihi, kodi ikisimamiwa vizuri kunakuwa na usawa, mwenye kipato kidogo wanalipa kidogo na wenye kipato kikubwa walipe kikubwa,” alisema Mwenda.

Aidha, alisema kuna baadhi ya wafanyabiashara wanaamini kuwa wafanyabiashara wakubwa hawalipi kodi wanayostahili kama wale wadogo.

Hivyo alisema kuanzishwa kwa kituo cha huduma kwa wateja Masaki ni uthibitisho wa kutosha kuwa hata wafanyabaishara wakubwa wanalipa kodi kama walipakodi wengine.

Kamishna alisema wanatarajia mamlaka hiyo itakuwa na vituo kama hivyo 71 nchi nzima ili iwe rahisi kuwafikia wateja wake wa aina zote kuwarahishia ulipaji kodi kwa hiyari kwa kuwapa elimu.

Pia Kamishna Mwenda aliwataka wafanyabiashara kuendelea kutumia mfumo wa IDRAS kwani mfanyabiashara halazimiki kwenda ofisi za TRA kupata huduma za kikodi badala yake anatumia mfumo huo kufanya shughuli zake zote mwenyewe akiwa ofisini kwake.

Alisema mfumo huo unapatikana saa 24 na mteja anaweza kujihudumia mwenyewe kwa kuomba marejesho ya kodi kwa kutumia mfumo au kuomba msamaha wa kodi kwa kutumia mfumo.

“Unaweza kuandika barua au kuomba ufafanuzi wowote, ni mfumo ambao umekuja kuleta mabadiliko makubwa sana ya usimamizi wa kodi nchini, hivyo kama unachangamoto ya mfumo wa IDRAS watumishi wetu wako nchi nzima nenda ukahudumiwe,” alisema

Aliwapongeza walipa kodi wa mkoa wa Kinondoni kwa namna ambavyo wanalipa kodi kwa hiyari hali ambayo imeuwezesha mkoa huo kufanya vizuri sana kwenye ukusanyaji wa mapato.

“Pia nawapongeza watumishi wa mamlaka kwa kutoa huduma nzuri ambazo zimewawezesha biashara zenu ziendelee kukua na nawahakikishia watumishi watakaokuwa kwenye kituo hiki wana weledi wa kutosha watawasadia,” alisema

Kwa upande wake Katibu tawala wa wilaya ya Kinondoni Bi. Warda Obathany amesema wilaya ya Kinondoni inakabiliwa na migogoro mingi ya ardhi inayotokanana mauziano ya ardhi na majengo na kuiomba TRA kuingilia kati kufuatilia mauziano hayo ili pia wakusanye kodi.

Amesema ofisi yake ipo tayari kutoa ushirikiano kwa TRA wakati wowote ili kuwezesha ukusanyaji wa kodi ambao umekuwa na manufaa makubwa kwa maendeleo ya nchi kwa kujenga miradi ya maji, umeme na miundombinu ya barabara huku ikitumika kutobesha hudma za afya.