MUSOMA KUNUFAIKA NA MRADI WA KISASA WA UWANJA WA NDEGE

Na Mwandishi Wetu,Musoma

WAZIRI wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, leo tarehe 23 Februari, 2026 amefanya ziara ya kikazi kukagua maendeleo ya Mradi wa Ujenzi na Uboreshaji wa Uwanja wa Ndege wa Musoma na kuagiza kuongeza kasi ya utekelezaji huku akisisitiza kuzingatiwa kwa viwango vya kitaifa na kimataifa vya usalama wa anga.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya mradi na kukagua eneo la ujenzi, Waziri Mbarawa amesema mradi huo ni wa kimkakati kwa Mkoa wa Mara na Taifa kwa ujumla, na unapaswa kukamilika ndani ya muda uliopangwa bila kuathiri ubora.

Ameeleza kuwa Mara ni mkoa wenye historia kubwa lakini haukuwa na uwanja wa ndege wa kiwango cha lami, hali iliyochochea Serikali kutumia fedha za ndani kugharamia mradi huo ili kuunganisha na mikoa mingine kupitia usafiri wa anga.

Kwa mujibu wa Waziri, uwanja huo wenye urefu wa kilomita 1.705 unagharimu shilingi bil. 36.3 na upo katika hatua nzuri za utekelezaji kwani mpaka sasa umefikia asilimia 60.

Amesema kazi za msingi zimekamilika na ndani ya miezi miwili mradi unatarajiwa kukamilika na kuanza kuhudumia ndege za masafa mafupi kama Q300, Q400 na ATR, huku majaribio yakitarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Aidha, Waziri amesema hatua itakayofuata ni kutafuta fedha kwa ajili ya kufunga taa za kuongozea ndege ili uweze kufanya kazi saa 24 kwa siku 7 za wiki, kujenga jengo la kisasa la abiria na uzio wa ulinzi, na baada ya hapo ni kuanza maboresho ya uwanja wa ndege wa Serengeti ili kuufungua zaidi Mkoa wa Mara kiuchumi.

Akitoa salamu za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Alfredi Mtambi amesema kukamilika kwa mradi huo kutachochea ajira, kukuza utalii na biashara katika Kanda ya Ziwa.

Awali, Msimamizi wa mradi, Mhandisi Ezra Magogo kutoka TANROADS, amesema ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege umeshakamilika kilichobaki ni kuweka michoro tu na kazi zinazoendelea kumaliziwa ni ujenzi wa apron, barabara za maingiliano, mifereji ya maji na kituo cha zimamoto

Naye Mbunge wa Musoma Mjini, Mhe. Mgore Miraji, ameishukuru Serikali kwa uwekezaji huo na kueleza kuwa wananchi watanufaika kupitia ajira, biashara na ukuaji wa sekta ya utalii.