Na Mwandishi Wetu,Pwani
MCHUNGAJI wa Kanisa la Kiinjiri Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kijitonyama Dk. Eliona Kimaro amesema serikali yoyote duniani haiwezi kuajira wahitimu wote katika nchi husika lazima kuwe na miradi ya familia ambayo itaweza kuwasaidia vijana kujiajiri na kuajiri.
Kauli hiyo ameitoa leo Machi, 7 2026 mkoani Pwani n wakati wa mahafali ya nane ya kidato cha nne mwaka 2025 ya shule hiyo iliyokuwa na lengo la kuwapongeza jumla ya wanafunzi 100 kwa ufaulu wa daraja la kwanza kwa wanafunzi wote.

Amesema kuwa miradi ya familia ndio suluhisho la ajira duniani kote hivyo wana jamii wanapaswa kuendeleza maono ya miradi yao ili kuweza kujipatia maendeleo.
“Waajiriwa mkifika nyumbani msipendelee kuangalia Tv ila hesabu siku zako za kustaafu na baada ya kustaafu unaenda wapi? Lazima uwe na mradi wa kuendeleza ukistaafu kazi na kuhimiza uchumi unaotokana na miradi ya familia,”amesema.

Amewaomba viongozi serikalini, dini na wengine kuendelea kuhamasisha juu ya miradi ya kifamilia ndio mwarobaini wa kutuondolea vijana mtaani.
Pia amewasihi wanafunzi wa shule ya Sekondari Christon kuendelea kuwa na nidhamu bora kwenye maisha kwa sababu ni hatma ya maisha yao.
“Maisha ni nidhamu na nidhamu ni maisha nidhamu ni msingi wa mafanikio katika maisha. Mwanafunzi mwenye nidhamu huheshimu walimu, wazazi na wenzake, hufuata sheria za shule, na hutumia muda wake vizuri kusoma,”amesema.

Pia amewaomba wazazi kuendelea kusimamia maadili dunia ya leo inapoteza wanaume kutokana na sayansi na teknolojia.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shule ya Sekondari Chriton, Enrique Msuya amesema wanafunzi wamepata fursa ya kujinza kwa vitendo kuhusu kilimo, ufugaji na uzalishaji wa chakula cha wanyama.

“Lengo letu ni kuhakikisha wanafunzi tunawapatia maarifa kwaajili ya ujasiriamali na kuelewa thamani ya uzalishaji katika uchumi ,”amesema.
Amesema wanaendelea kujenga mazingira bora kwa wanafunzi na waalimu kwa kutoa elimu kwa uadilifu, nidhamu na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Awali akizungumza kuhusu mafanikio ya shule hiyo, Mkuu wa Shule, Augustin Minja amesema mafanikio hayo yametokana na msisitizo mkubwa wa nidhamu, juhudi za walimu pamoja na ushirikiano wa wanafunzi katika kujifunza.
Amesema tangu kuanzishwa kwa shule hiyo mwaka 2015, uongozi umejikita katika nguzo nne muhimu, ambazo ni Mungu kwanza, nidhamu, taaluma na ujasiriamali. Nguzo hizo zimekuwa msingi muhimu katika kuwajenga wanafunzi kitaaluma na kimaadili.

“Uongozi wa shule umeweka msisitizo mkubwa katika kudhibiti tabia zisizofaa. Shule hiyo haivumilii vitendo vya utovu wa nidhamu, ikiwemo matumizi ya madawa ya kulevya na mienendo mingine inayokiuka maadili ya shule. Kwa mujibu wa uongozi wa shule, kila mwanafunzi anatakiwa kuzingatia nidhamu bora ili kufikia mafanikio katika masomo na maisha ya baadaye,” amesema.
Minja amesema kuwa ufaulu mzuri wa wanafunzi unatokana na nidhamu pamoja na mazingira mazuri ya kujifunzia, akisisitiza kuwa vijana wanaosoma shuleni hapo ni nguvu kazi na viongozi wa taifa la kesho.
Mbali na masomo ya kawaida darasani, shule pia imeweka mkazo katika elimu ya vitendo kwa kufundisha masomo kama kilimo, muziki na michezo. Lengo la mpango huo ni kuwajengea wanafunzi ujuzi wa kujitegemea na kuwafanya kuwa wajasiriamali tangu wakiwa shuleni.

Amesema kupitia somo la kilimo, wanafunzi hujifunza thamani ya mazao mbalimbali pamoja na mbinu za uzalishaji, jambo linalowawezesha kuwa na uwezo wa kujiajiri baada ya kuhitimu masomo yao.
Mpango huo pia unaendana na Sera ya Elimu ya mwaka 2014, toleo la 2023, inayosisitiza kutoa elimu yenye vitendo ili kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujitegemea katika maisha yao ya baadaye.
Kwa ujumla, uongozi wa shule unaamini kuwa mchanganyiko wa nidhamu, elimu bora na mafunzo ya vitendo utaendelea kuwa msingi wa kuwalea wanafunzi wenye uwezo wa kuchangia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.


