VIPENGELE 41 KUING’ARISHA TANZANIA TUZO ZA UTALII NA USAFIRISHAJI DUNIANI

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

TANZANIA imeingiza vipengele 41 katika Tuzo za Utalii na Usafirishaji Duniani (World Travel Awards), hatua hiyo  inaimarisha nafasi yake na kukua zaidi katika sekta ya  ya utalii  na kuwa kinara barani Afrika

Akizungumza leo Aprili 11,2026 jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Paulina Mkama, amesema tuzo hizo zinahusisha jumla ya washindani 85 kutoka sekta za umma na binafsi.anbapo pamoja na mambo mengine  zinalenga kutambua na kusherehekea ubora wa huduma, kuhamasisha ushindani  na zinatoa  fursa kwa wadau na watalii kupigia kura vivutio bora duniani.

” Ushiriki wa Tanzania katika tuzo hizo ni fursa adhimu ya kuitangaza nchi kimataifa na kuiweka katika ramani ya dunia kama kitovu cha utalii,taasisi  serikali, ikiwemo TFS (Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania) na TAWA (Mamlaka ya Wanyama ya Usimamizi wa Wanyama Pori Tanzania), zimefanikiwa kuwasilisha vivutio vyake katika kinyang’anyiro hicho.

“Kwenye kinyang’anyiro hicho , Tanzania imewania nafasi katika vipengele mbalimbali barani Afrika, huku vivutio vikubwa kama Hifadhi ya Taifa ya Serengeti vikitajwa kuwania tuzo za juu,”alisema Mkama.

Alisema ili kuwezesha vivutio hivyo kupata ushindi TTB imeanzisha  kampeni ya “Kura Moja, Tiketi Moja kwa Tanzania” inaendelea.ambapo Watanzania na wadau wa utalii wakihamasishwa kushiriki kikamilifu kupigia kura nchi ili kuongeza nafasi ya ushindi.

 Amesema katika baadhi ya vipengele, washindani saba kati ya 14 wanatoka Tanzania, hali inayoonesha uimara na ushindani wa sekta ya utalii nchini.

Amesisitiza kuwa sekta ya utalii inachangia zaidi ya ajira milioni moja kila mwaka, na mafanikio katika tuzo hizi yataongeza fursa za uwekezaji, ajira pamoja na kukuza pato la taifa.

“Mbali na kuimarisha ushindani wa ubora wa huduma, tuzo hizo pia huchochea ukuaji wa sekta ya utalii kupitia ubunifu, uwekezaji na kuongeza mvuto wa vivutio katika soko la kimataifa,” amesema Paulina.

Ameongeza kuwa  kwa mara ya kwanza, baadhi ya vivutio vinavyosimamiwa na taasisi za serikali kama TAWA na TFS ikiwemo Mpanga Kipengere, Aman Forest Reserve, Selous Game Reserve, Pugu Kazimzumbwi na Kilwa Kisiwani, vimeingia kwenye ushindani huo, jambo linaloashiria kukua kwa sekta ya utalii nchini.