MSHINDI WAZO BUNIFU KUKABIDHIWA SH MILIONI 50

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

VIJANA wakitanzania wametakiwa kushiriki kutoa mawazo bunifu yenye lengo la kutoa suluhisho ya mambo yanayoikabili jamii  ambapo mshindi wa wazo hilo atapewa zawadi ya Sh Milioni 50.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam juzi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka wakati akiwatangazia vijana kushiriki Shindano kubwa la Kitaifa la kutoa mawazo bunifu yenye lengo la kutoa suluhisho ya mambo yanayoikabili jamii.

Alisema baada ya mashindano madogo madogo ambayo walikuwa wakiyafanya katika mikoa kupitia jukwaa la vijana, sasa watakuwa na shindano kubwa la kitaifa ambalo litakuwa na zawadi kwa vijana ambao watashiriki kutoa mawazo hayo.

Waziri Nanauka alisema shindano hilo wamelipa jina la Vijana Uchumi Chanya, likiwa na kauli mbiu ‘Wana wanafikiri Taifa Linasonga’.

“Tumeshihudia dunia imengia katika mabadiliko makubwa ya kisiasa kiuchumi na kijamii ambayo yanasababishwa na migogoro ya kimataifa ikiwemo vita kwa baadhi ya mataifa na kumekuwa na ushindani mkubwa wa kiuchumi baina ya mataifa hayo na kasi pia ya teknolojia katika kushughulikia mambo mbalimbali,”alisema Nanauka.

Waziri Nanauka alisema mabadiliko hayo yameibua mazingira mapya ya kiuchumi ya duniani ambayo yanaathiri kwa namna moja au nyingine uchumi wa mataifa mengine hususan yale yaliyoendelea ikiwemo Tanzania katika sekta mbalimbali.

Alisema kwa Tanzania hali hiyo imeleta umuhimu mkubwa kwa kutumia kikamilifu rasilimali ya vijana ambayo ni nguvu kazi kubwa katika Taifa asilimia 55.6 ya nguvu kazi ya Taifa ni vijana kuanzia umri wa miaka 15 hadi 35. 

Aidha, alieleza kuwa vijana wana uwezo mkubwa wa ubunifu, fikra mpya na mtazamo mpana unaoweza kusaidia taifa kukabiliana na changamoto hizo na kuimarisha uchumi wake.

Alisema kwa kutambua umuhimu wa shindano hilo Wizara imetenga Sh milioni 50 zitakazotolewa kwa washindi na ili kuhakikisha shindano hilo linakuwa la vijana wenyewe kwa mamalaka aliyokuwa nayo na kwa mujibu wa sheria ameunda kamati ya Kitaifa ya Vijana 11.

Alieleza kuwa kamati hiyo itakuwa na jukumu la kuweka utaratibu wa ushiriki kwa mujibu wa muongozo wa wizara, kuratibu upokeaji wa mawazo ya vijana kutoka maeneo yote ya nchi, kutoa elimu na hamasa kwa vijana kuhusu namna ya kushiriki, kuchagua majaji wabobezi watakaoamua washindi, pamoja na kuratibu maandalizi ya shughuli zote za shindano hilo hadi kilele chake.

“Dhamira yetu ni kuona yule anayestahili ndiye anashinda. Tumeweka vigezo na taratibu za kuhakikisha hakuna upendeleo wa aina yoyote na kila kijana anapata nafasi sawa kulingana na uwezo wake,” alisisitiza.

Alisema Mwenyekiti wa Kamati hiyo ni Joseph Malekela ni kiongozi kijana mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 10 katika kuchagiza ushiriki wa vijana katika mchakato wa maamuzi, amani, usalama na maendeleo.

Kwa upande wake, Malekela alisema shindano hilo litafanyika kwa uwazi, lakini pia kwa kuwa nchi ni kubwa watafanya kila wanaloweza hata wale vijana waliyokuwa maeneo ya pembezoni waweze kuwafikia kwa kuwafikishia taarifa ya shindano hilo.