Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 1,983.31 za dawa mbalimbali za kulevya, kilogramu 3,012.5 na lita 17,960 za kemikali bashirifu, vidonge 286 na chupa 1,001 za dawa tiba zenye asili ya kulevya katika kipindi cha mwezi Machi 2026.
Aidha katika ukamataji huo uchambuzi wa takwimu umebaini ongezeko la ukamataji wa dawa za kulevya aina ya mirungi ambapo kilogramu 1,267.12 zilikamatwa, sawa na 64 ya dawa zote zilizokamatwa mwezi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Kamishna Mkuu wa DCEA Aretas Lyimo alisema katika operesheni hiyo ha mwezi Machi wamekamata ekari 55.5 za mashamba ya bangi na kuziteketezwa pamoja na magari tisa, pikipiki 12 na bajaji moja vilikamatwa huku watuhumiwa 77 wakikamatwa kuhusiana na makosa hayo.
Alisema katika ukamataji huo uchambuzi wa takwimu umebaini ongezeko la ukamataji wa dawa za kulevya aina ya mirungi .

Alisema hali hiyo imetokana namkakati wa DCEA kujikita katika operesheni za dawa za kulevya za mashambani baada ya kudhibiti kwa kiasi kikubwa mitandao ya dawa za kulevya za viwandani.
“Baadhi ya matukio ya ukamataji yaliyofanyika katika maeneo mbalimbali nchini ni kama ifuatavyo,jijini Dar es Salaam, katika eneo la Tegeta Kibo, kilogramu 101.2 za mirungi zilikamatwa zikiwa zimefichwa katika basi la abiria aina ya Yutong la kampuni ya Abood lenye namba ya usajili T 181 EMJ lililokuwa likifanya safari kati ya Mombasa, Kenya na Dar es Salaam, Tanzania.

“Dawa hizo zilifichwa katika maeneo mbalimbali ya basi hilo ikiwemo ndani ya mfumo wa hewa (AC) kwa lengo la kukwepa kugundulika,watuhumiwaaliokamatwa katika tukio hilo ni dereva wa basi hilo Ramadhan Mohamed (52), Salma Sanga (26) kondakta,Twahilu Athuman (38), Mohamedy Mikidadi (37) na Ibrahim Mohamed (39).
“Mkoani Pwani kilogramu 419.09 za mirungi zilikamatwa zikiwa zinasafirishwa kuelekea Dar es Salaam,katika mkoa wa Mwanza, zilikamatwa kilogramu 52 za mirungi katika kizuizi cha barabarani cha Magu pamoja na
Bandari ya Mwanza South, ikisafirishwa kwa kutumia gari aina ya Fuso yenye namba ya usajili T 296 APA,”alisema Kamishna Lyimo.
Alisema dawa hizo zilikuwa zimefichwa katikati ya mizigo mingine, ikiwemo mabelo ya nguo za mitumba ambapo dereva wa
gari hilo, Hassan Hassan (37), mkazi wa Mahina Nyamagana walikamatwa.

Mbali na watuhumiwa hao wilayani Misungwi mkoani humo kilogramu 184.9 za mirungi zilikamatwa zikiwahusisha watuhumiwa Chrispin Shoo (62) na mkewe Esther Pastory (55).
” Dawa hizo zilibainika ndani ya nyumba na katika vyombo vya usafiri ambavyo ni Gari aina ya Toyota Crown yenye namba ya usajili T 742 EGL, Toyota Wish yenye namba ya usajili T 854 DXB, pamoja na bajaji yenye namba za usajili MC 261 EZV.

“Mkoani Tanga, zilikamatwa Kilogramu 32.95 za Mirungi ikiwa imefichwa ndani ya mfuko kwa kuchanganywa na maembe,katika tukio hilo, Seif Omar (38), maarufu kwa jina la Haniwao, mkazi wa Mtaa wa Taifa Barabara ya 13, ambaye pia ni mjumbe wa Serikali ya Mtaa alikamatwa,”alisema Kamishna Lyimo.
Alisema katika operesheni nyingine zilizofanyika mkoani humo, jumla ya Kilogramu 164.01 za Mirungi zilikamatwa katika matukio tofauti vilevile, mkoani Arusha, katika wilaya ya Longido, Kilogramu 106.25 za mirungi zilikamatwa zikiwa zinasafirishwa kwa gari aina ya Toyota Wish yenye namba ya usajili T 889 DPG. Katika tukio hilo ambapo watuhumiwa ni Solomon Koholo (38), Diwani wa Kata ya Kimokouwa pamoja na Lekaneti Kukuu (38) walikamatwa.
Alisema pia kilogramu 138.42 za dawa za mirungi zilikamatwa katika matukio mengine yaliyofanyika mkoani humo kadhalika mkoani Kilimanjaro, katika eneo la Himo na Same, Kilogramu 68.3 za mirungi zilizowahusisha watuhumiwa Amin Mazua (58) maarufu kwa jina la Mbaruku na Wilbard Mchau (50).

Alisema sambamba na udhibiti wa mirungi, aina nyingine ya dawa za kulevya zilikamatwa katika maeneo mbalimbali
nchini ambapo jijini Dar es Salaam, kwenye hosteli ya wanafunzi iliyopo mtaa wa Nzasa, Kijitonyama zilikamatwa Paketi 141 za bangi aina ya skanka.
“Katika tukio hilo, alikamatwa mtuhumiwa Semvua Sangi (31), msimamizi wa hosteli
hiyo ambaye dawa hizo zilipatikana ndani ya chumba chake katika hosteli hiyo. Tukio hili linaashiria uwepo wa
mienendo ya biashara ya dawa za kulevya katika maeneo yanayozunguka taasisi za elimu.
” Mamlaka inatoa wito kwa jamii, hususani wamiliki na wasimamizi wa makazi ya wanafunzi, kushirikiana na vyombo vya dola
kuhakikisha mazingira ya wanafunzi yanabaki salama bila dawa za kulevya,”alisema Kamishna Lyimo.
Aidha, mkoani Songwe katika eneo la Tunduma, zilikamatwa Kilogramu 8.2 za bangi aina skanka dawa hizo
zilibainika zikiwa zinasafirishwa na mtuhumiwa Lwitiko Kapambila (39) kuelekea Mbeya mjini, akiwa ndani ya lori aina ya FAW alilokuwa ameomba lifti kutokea Tunduma.

Alisema katika operesheni nyingine zilizofanyika nchini, jumla ya kilogram 707.995 za bangi zilikamatwa.
Aidha katika kuimarisha udhibiti wa kemikali bashirifu na kuzuia uchepushwaji wa dawa tiba zenye asili ya kulevya DCEA kwa kushirikiana na Mamlaka nyingine za udhibiti ilifanya ukaguzi katika kampuni zinazojihusisha na
kemikali bashirifu, maduka ya dawa tiba, kampuni za usafirishaji vifurushi na bandari kavu.
“Kutokana na ukaguzi huo, jumla ya kilogramu 3,012.5 na lita 17,960 za kemikali bashirifu zilizuiliwa kutokana
na kukiuka taratibu mbalimbali za kisheria. Miongoni mwa Kemikali hizo ni Potassium permanganate,Hydrochloric acid, Acetone, Sulphuric acid, na Acetic acid glacial.
“Kemikali hizi endapo zingechepushwa
zingeweza kutumika katika mchakato wa kuzalisha dawa za kulevya,”alisema Kamishna Lyimo.

Alisema pia kupitia ukaguzi huo, vidonge 286 na chupa 1,001 za dawa tiba zenye asili ya kulevya vilikamatwa ambapo dawa
hizo ni alprazolam, midazolam, clonazepam, Fentanyl, zolpidem, Tramadol, Codeine na dihydrocodeine.
“Kitaalam, dawa hizi zinajumuisha makundi ya Benzodiazepini, dawa za kutuliza na kusababisha usingizi,pamoja na dawa zenye asili ya afyuni ambazo hutumika kutibu maumivu. Endapo matumizi ya dawa hizi hayatadhibitiwa ipasavyo zinaweza kusababisha uraibu na utegemezi kwa mtumiaji sawa na dawa za kulevya,”alisema Kamishna Lyimo.


