DK. NCHIMBI KUZINDUA MKAKATI WA MAGEUZI YA MAZINGIRA NCHINI

Na Asha Mwakyonde, DODOMA

MAKAMU wa Rais, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yatakayofanyika kesho kwa niaba ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambapo pia atazindua Mkakati wa Mageuzi Kabambe ya Usimamizi wa Mazingira nchini.

Hayo yamesemwa leo Juni 4, 2026, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yusuf Masauni, baada ya kukagua mabanda mbalimbali katika maonesho ya Wiki ya Mazingira yanayoendelea jijini Dodoma.

Masauni amesema uzinduzi wa mkakati huo ni hatua muhimu katika kuimarisha juhudi za Serikali za kukabiliana na changamoto za mazingira na kutafuta suluhisho endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Ametoa wito kwa wananchi ambao bado hawajapata fursa ya kutembelea maonesho hayo kujitokeza kabla ya kuhitimishwa kwake, akieleza kuwa kuna mambo mengi ya kujifunza pamoja na bidhaa na teknolojia mbalimbali zinazohusiana na uhifadhi wa mazingira.

Amefafanua kuwa maonesho hayo yanaenda sambamba na shughuli mbalimbali zinazolenga kuhamasisha utunzaji wa mazingira katika kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yatakayohitimishwa kesho.

“Kwa yale niliyoyaona hapa na ushiriki mkubwa wa taasisi za Serikali na sekta binafsi, dhamira ya Serikali ya kutafuta na kutoa majawabu ya changamoto za mazingira inaonekana wazi. Tukishirikiana kwa pamoja tutafanikiwa kuyatatua matatizo haya,” amesema Masauni.