DCEA KUSHIRIKIANA NA VETA KUWAPA MAISHA MAPYA WANAOACHA DAWA ZA KULEVYA

Na Aziza Masoud,Dar es Salam

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesaini makubaliano na Chuo Cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi(VETA)  kuwasaidia waraibu wa dawa za kulevya wanaopata nafuu  kupata elimu ya ufundi stadi  kwa bei nafuu katika vyuo vilivyopo nchi nzima.

Akizungumza leo Juni 4. 2026 wakati wa kusaini makubaliano hayo Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo alisema serikali kupitia DCEA imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kudhibiti na kupambana na tatizo la dawa za kulevya  ikiwemo kuzuia biashara hiyo haramu kutoa elimu kwa jamii, pamoja na kuimarisha huduma za tiba na urejeshaji wa waraibu wa dawa za kulevya katika jamii.

Amesema hata hivyo uzoefu unaonyesha kuwa matibabu pekee hayatoshi ikiwa mhusika atapatiwa mazingira bora ya kujijenga katika maisha ya kawaida,watu wengi wanaopona uraibu hukumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ajira, kipato, na wakati mwingine kujenyepaliwa na jamii. 

“Changamoto hizo zinaweza kuwafanya kurejea tena kwenye matumizi ya dawa za kulevya endapo hawatakuwa na shughuli yoyote ya kufanya na endapo pia serikali inakuwa haijawapatia mbadala wa kitu cha kufanya mwisho wa siku wanajikuta wanarudi tena kwenye matumizi ya dawa za kulevya.

“Ndiyo maana leo tunatoa umuhimu mkubwa kwa ushirikiano huu kati ya DCEA na Veta, kupitia hati hii ya makubaliano,waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu watapata nafasi ya kujiunga na vyuo mbalimbali vya Veta nchini kwa gharama nafuu ili kuweza kujifunza ujuzi wa kazi mbalimbali kama vile ufundi selemala, umeme, ushonaji, ufundi magari, sehama, upishi, na taaluma nyinginezo zinazowezesha kujitegemea,”amesema Kamishna Lyimo.

Amesema matarajio  ya serikali ni kwamba baada ya kuhitimu mafunzo hayo, wahitimu hao watawezeshwa kwa vifaa vidogo vya kuanzia kazi kulingana na ujuzi walioupata ili waweze kuanza shughuli za uzalishaji na kujipatia kipato.

Amesema  DCEA itaendelea kushirikiana na taasisi za fedha zinazotoa mikopo midogo midogo yaani microfinance ili kuunganisha wahitimu hao na fursa za mitaji kwa ajili ya kuanzisha biashara na shughuli mbalimbali za kiuchumi ili waweze kujipatia kipato. 

“Mpango huu una umuhimu mkubwa kwa sababu unalenga kuwajengea uwezo waraibu waliopona ili waweze kuwa sehemu ya maendeleo ya jamii badala ya kubaki kuwa tegemezi kwa jamii,tunaamini kuwa mtu anayekuwa na ujuzi ajira au kipato halali huwa na nafasi kubwa zaidi ya kuendelea kuwa salama, dhidi ya kurejea kwenye matumizi ya dawa za kulevya,”amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Amesema  mpango huo utatekeleza kwa dhana ya kuwapa nafasi ya pili katika maisha waraibu waliopata nafuu wanahitaji kuungwa mkono wakiwa moyo na kuaminiwa, ili kuweza kujenga upya maisha yao na kurejesha heshima yao katika jamii.

Naye  Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA Antony Kasore amesema  utekelezaji wa mpango huu muhimu una lengo la kuwasaidia waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu ili kujijengea maisha mapya yenye matumaini na jipya kwa taifa letu.

Amesema makubaliano hayo waliyosaini ni muhimu  kwa VETAna DCEA  ili kuwasaidia vijana wetu na ndugu zetu ambao walijihusisha na matumizi ya Madawa ya  kulevya (warahibu) lakini kwa jitihada mbalimbali wameweza kutibiwa na  sasa wapo tayari  kuendelea kujenga Taifa.

” Hivyo  waraibu hao watapatiwa Mafunzo ya Ufundi Stadi ili waweze kajiriwa, kujiajiri na ikiwezekana na wao kuajiri wengine, jambo ambalo badala ya kutengwa na jamii litaongeza ushiriki wao katika shughuli mbalimbali za jamii.

‎”Tukio hili la leo linathibitisha utayari wa VETA kulitekeleza suala hili kwa lengo la kuisaidia Serikali na jamii kwa ujumla kwa kuwaongezea thamani kwa jamii warahibu wote. Pia wapo  warahibu ambao walishapata ujuzi kwa njia mbalimbali  kwa mfumo usio rasmi,  na ambao watahitaji kurasimisha ujuzi wao,  VETA ipo tayari kuwarasimisha na kuwapatia vyeti kwa lengo la kuufanya ujuzi wao uweze kutambuliwa,”amesema CPA Kasore.