Na Mwandishi Wetu,Dodoma
WANANCHI wametakiwa kutumia Bima ya Maisha ya Majaliwa kama njia ya kujiwekea akiba na kutimiza malengo ya kifedha ya muda mrefu, huku wakihakikishiwa ulinzi wa familia zao endapo watapata matatizo kabla ya kufikia malengo hayo.
Wito huo umetolewa na Afisa Bima wa NIC Insurance, Thecla Mtege, alipokuwa akizungumza na wananchi waliotembelea banda la kampuni hiyo katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea kwenye Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.

Thecla alisema Bima ya Maisha ya Majaliwa inampa mwananchi nafasi ya kupanga malengo ya kifedha kwa kipindi anachokihitaji, kuanzia miaka mitano, 10 au zaidi, huku akichangia fedha kidogo kila mwezi kulingana na uwezo wake.
Alisema mfumo huo unamwezesha mwananchi kujenga akiba kwa ajili ya mahitaji ya baadaye, yakiwemo elimu ya watoto, ujenzi wa nyumba, mtaji wa biashara au maandalizi ya maisha ya baadaye.

“Mwananchi anaweza kuanza na kiasi anachokimudu kila mwezi na kuendelea kujenga akiba itakayomsaidia kutimiza malengo aliyojiwekea,” alisema.
Aliongeza kuwa pamoja na kuwa chombo cha kuweka akiba, bima hiyo pia inalinda familia ya mteja endapo atafariki kabla ya muda wa mkataba kuisha.
Kwa mujibu wa Thecla, katika mazingira hayo NIC Insurance hulipa kiwango cha bima kilichokubaliwa kwa wategemezi waliotajwa na mteja, hatua inayosaidia familia kuendelea kupata msaada wa kifedha licha ya kumpoteza mpendwa wao.

Alisema huduma hiyo ni miongoni mwa bidhaa zinazolenga kuwajengea wananchi utamaduni wa kupanga fedha zao mapema huku wakijihakikishia usalama wa kifedha wao na familia zao.


