e-GA: MIFUMO YA KIDIGITALI YA KILIMO  INAONGEZA UWAZI 

Na Aziza Masoud,Dodoma

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA)  inaendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo katika kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali inayorahisisha utoaji wa huduma, kuongeza uwazi na kuboresha usimamizi wa shughuli za kilimo nchini.

Akizungumza katika Maonesho ya Wakulima  ya Kitaifa yanayoendelea jijini Dodoma, Meneja wa Mawasiliano e -GA  Subira Kaswaga alisema taasisi hiyo imeshiriki katika ujenzi wa mifumo mbalimbali ya sekta ya kilimo, ikiwemo mfumo unaowezesha Wizara ya Kilimo kupata taarifa za wakulima nchini, kufuatilia shughuli za taasisi zilizo chini ya wizara hiyo na kutoa taarifa muhimu za kilimo kwa wadau.

Aliongeza mamlaka hiyo imeshirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika kutengeneza Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika unaojulikana kama MUVU, unaosaidia kuongeza uwazi katika uendeshaji wa vyama hivyo pamoja na kuwawezesha wakulima kufuatilia mauzo ya mazao yao, bei na malipo wanayostahili kupata.

“Hadi sasa zaidi ya vyama 6000 vya ushirika vinatumia mfumo huo, jambo lililosaidia kuboresha usimamizi wa mapato na kuongeza uwajibikaji katika sekta ya ushirika.

Alisema mamlaka hiyo ina jukumu la kuandaa na kusimamia mifumo mbalimbali ya TEHAMA inayotumika serikalini ili kuboresha utendaji kazi wa taasisi za umma na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Alieleza kuwa e-GA imeshirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuanzisha Fertilizer Information System (FIS), mfumo unaowezesha kusimamia wazalishaji na waingizaji wa mbolea, kufuatilia mwenendo wa soko na kuhakikisha wauzaji wanazingatia bei elekezi zinazotolewa na Serikali.

Alisema mfumo huo unaisaidia Serikali kudhibiti soko la mbolea ili wakulima waweze kupata pembejeo hizo kwa bei stahiki na hivyo kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.

Mbali na mifumo hiyo, taasisi za sekta ya kilimo zinaendelea kutumia mifumo mingine ya Serikali ikiwemo barua pepe za Serikali (Government Email System) na Mfumo wa Ofisi Mtandao, ambayo imeboresha mawasiliano na utendaji kazi ndani ya taasisi za umma.

Mamlaka hiyo imewataka wananchi kutembelea banda la e-GA katika maonesho yanayoendelea Dodoma ili kujifunza zaidi kuhusu mifumo ya kidijitali inayotumika kuboresha utoaji wa huduma za Serikali na mchango wake katika maendeleo ya sekta ya kilimo.