Na Mwandishi Wetu, Dodoma
BODI ya Bima ya Amana (DIB) imewataka watu 428 ambao walikuwa wanachama wa benki ya FBME kwenda kuchukua fedha zao haraka ambazo ni takribani Sh Bilioni nne.
Akizungumza leo Agosti 2, 2026 jijini Dodoma katika Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima Nane Nane,Mkurugenzi Mkuu wa DIB,Isack Kihwili alisema madai ya wenye amana wa Benki ya FBME kwa upande wa Tanzania yalifikia takribani Sh Bilioni 35, hadi sasa zaidi ya asilimia 85 ya fedha hizo tayari zimeshalipwa kwa walengwa huku madai yenye thamani ya karibu Sh Bilioni nne wahusika wake wakiwa bado hawajajitokeza.

Alisema pamoja na kulipwa kwa madai hayo lakini bado kuna takribani watu 428 ambao hawajajitokeza kuchukua fedha zao zenye thamani ya karibu Sh Bilioni nne.
“Hizi fedha tayari tulishazitenga kwa ajili yao hivyo endapo kundi hilo litajitokeza na kulipwa, hatua inayofuata itakuwa ni kulipa asilimia 15 zilizobaki ili kila mwenye amana astahili kulipwa madai yake kwa asilimia 100,”alisema Kihwili.

Aidha aliongeza kuwa bado kuna kundi la wadai wengine, wakiwemo baadhi ya wafanyakazi waliokuwa na madai yaliyofikishwa mahakamani.
Alisema wadai hao malipo yao hayajahusishwa katika awamu inayoendelea kutokana na mchakato wa kuendelea kufuatilia na kuhakiki mali za benki hiyo.
Alisema DIB inaendelea kufanya kazi ya kufuatilia mali zilizobaki ili kuhakikisha fedha za kutosha zinapatikana kwa ajili ya kukamilisha malipo ya wadai hao kwa kuzingatia taratibu za kisheria.

Mbali na hilo Kihwila aliwataka wananchi kufika katika banda hilo ili kupata elimu kuhusu ulinzi wa amana zao na taratibu za kufidia fedha wanazoweka katika taasisi za fedha zenye leseni ya Benki Kuu ya Tanzania.
Amewataka wananchi kuendelea kuweka fedha zao katika taasisi zilizosajiliwa na zenye leseni ya Benki Kuu ya Tanzania ili waweze kupata haki zao endapo kutatokea tatizo ndani ya taasisi husika.


