Na Mwandishi Wetu, Dodoma
CHUO Cha Ufundi Stadi (VETA) Singida kimewahimiza wafugaji wa ng’ombe nchini kuongeza thamani ya maziwa wanayozalisha kwa kuyachakata na kutengeneza bidhaa mbalimbali badala ya kuyauza yakiwa mabichi, hatua ambayo itawaongezea kipato na kuinua thamani ya bidhaa zao.
Akizungumza katika banda la Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika Maonesho ya Wakulima ya Kimataifa Nanenane yanayofanyika kitaifa mjini Dodoma, mkufunzi kutoka VETA Singida, Dk. Crispin Mkopi,alisema ni wakati wa wafugaji kuongeza thamani katika maziwa na kutengeneza bidhaa kama mtindi, yoghurt na siagi anaweza kuongeza mapato yake kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na kuuza maziwa mabichi.

“Kwa kawaida lita moja ya maziwa huuzwa kati ya shilingi 1,500 na 2,000, lakini ikiongezwa thamani na kutengenezwa bidhaa mbalimbali inaweza kuingiza kati ya shilingi 5,000 hadi 6,000 kwa lita moja,” alisema.
Alieleza kuwa VETA Singida imeleta suluhisho la wafugaji kupitia maonesho hayo kwakutengeneza bidhaa mbalimbali zinazotokana na maziwa ikiwemo mtindi wa kawaida, yoghurt yenye ladha ya strawberry na vanilla pamoja na siagi, huku ikitoa mafunzo ya namna ya kuzitengeneza kwa kufuata viwango vya usafi na ubora.

Kwa mujibu wa Dkt. Mkopi, uzalishaji wa mtindi bora huanza katika hatua ya ukamuaji wa maziwa katika mazingira safi kwa kutumia vyombo salama, kisha maziwa huchemshwa hadi kufikia nyuzi joto 90 za Selsiasi na kuachwa yapoe kabla ya kuongezwa bakteria maalumu (culture) na viambato vingine kama ladha na rangi kwa ajili ya kutengeneza yoghurt.
Alisema baada ya hatua hizo, maziwa huwekwa katika mazingira yenye joto stahiki kwa saa nne hadi sita ili bakteria wafanye kazi ya kuyageuza kuwa yoghurt yenye ubora.

Aidha, aliwataka wafugaji kutumia teknolojia na elimu wanayoipata kupitia VETA ili kuongeza thamani ya mazao yao, akisisitiza kuwa hatua hiyo itawasaidia kupata soko lenye tija zaidi na kuongeza kipato cha kaya zao.
“Badala ya kuuza maziwa katika hali ya kawaida, wafugaji wajifunze kuyachakata na kuzalisha bidhaa mbalimbali zenye thamani kubwa sokoni. Hii ndiyo njia ya kuongeza kipato na kuimarisha uchumi wa mfugaji,” alisema.


