Na Mwandishi Wetu,Rukwa
WIZARA ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), imempokea rasmi nchini mhamasishaji amani duniani, Saddam Suleiman Ali Alaya (Mr. Alaya), anayetekeleza safari ya kihistoria ya The World’s Longest Peace Walk, inayolenga kuweka rekodi ya Guinness World Records kupitia matembezi marefu zaidi ya kuhamasisha amani na mshikamano wa kimataifa.
Mr. Alaya ameingia nchini Agosti 2,2026, kupitia Mpaka wa Kasesya uliopo Wilaya ya Kalambo, mkoani Rukwa, ambako ameanza rasmi safari yake ya takribani siku 35 nchini Tanzania.

Safari hiyo ni sehemu ya mradi wa kimataifa unaolenga kutembea zaidi ya kilomita 23,000 kutoka Cape Town, Afrika Kusini hadi Magadan, Urusi, kupitia nchi 18 kati ya mwaka 2026 na 2028. Tanzania ni nchi ya tano katika ratiba ya safari hiyo, ikiwa ni fursa ya kuitangaza nchi kimataifa kupitia vivutio vyake vya utalii, urithi wa asili, utamaduni na ukarimu wa Watanzania.
Mbali na kuhamasisha amani na mshikamano wa kimataifa, anatarajiwa kuitangaza Tanzania katika jukwaa la utalii duniani kupitia kampeni ya kimataifa ya utangazaji inayohusisha vyombo mbalimbali vya habari, utengenezaji wa makala maalumu na ushirikiano na mitandao ya kimataifa inayotarajiwa kufikia zaidi ya watu milioni 480.

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada zinazofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia TTB ambayo inatumia majukwaa ya kimataifa kuitangaza Tanzania kama moja ya nchi bora kwa utalii barani Afrika na duniani, huku ikiwakaribisha wageni kutoka kila pembe ya dunia kufika nchini kujionea vivutio vya kipekee vya asili, utamaduni na urithi wa Taifa.


