WAZIRI HOMERA AHIMIZA KASI YA UTEKELEZAJI WA MRADI UMEME SONGEA- TUNDURU NA TUNDURU- MASASI

šŸ“ŒAsema dhamira ya Serikali ni kuona wananchi wa kusini wananufaika na umeme wa uhakika

šŸ“ŒAtoa rai kwa TANESCO kumsimamia Mkandarasi kukamilisha mradi kwa wakati

Na Mwandishi Wetu,Songea

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Homera, amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Songea hadi Tunduru, wenye urefu wa kilomita 214, pamoja na ujenzi wa Kituo cha Kupokea, Kupoza na Kusambaza Umeme cha Tunduru, kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati.

Mradi huo unatarajiwa kuimarisha gridi ya Taifa na kunufaisha wananchi wa mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara kwa kuboresha upatikanaji wa umeme na kuchochea shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Waziri Homera ametoa agizo hilo Oktoba 25, 2026, wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya mradi huo, ambao unatekelezwa katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Songea hadi Tunduru, ikijumuisha ujenzi wa Kituo cha Kupokea, Kupoza na Kusambaza Umeme cha Tunduru, huku sehemu ya pili ikiwa ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Tunduru hadi Masasi, yenye urefu wa kilomita 177.

ā€œNimeona maendeleo ya mradi. TANESCO, msimamieni mkandarasi ili aweze kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi. Dhamira ya Serikali ni kuona wananchi wa mikoa ya kusini wananufaika na uwekezaji katika sekta ya umeme ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika shughuli za kichumi na kijamii’’alifafanua Waziri Homera.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Naibu Mkurugenzi Mtendaji anayeshughulikia Mipango, Utafiti na Uwekezaji, Mhandisi Amos Kaihula, amesema utekelezaji wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Songea hadi Masasi umefikia asilimia 56, huku mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Tunduru hadi Masasi ukiwa umefikia asilimia 34.

ā€œUtekelezaji wa miradi hii ni muhimu kwa kuwa inalenga kuhakikisha wananchi wa mikoa ya Kusini wananufaika na umeme wa uhakika. Tunafanya jitihada kubwa za kumsimamia mkandarasi ili aweze kukamilisha kazi kwa wakati na kwa ufanisi, kwa maslahi ya maendeleo ya nchi na Taifa kwa ujumla,ā€ alieleza Mhandisi Kaihula.

Mradi huo, unatekelezwa na Kampuni ya Kalpataru Projects International Limited kutoka India ambapo sehemu ya kwanza ya mradi kutoka Songea hadi Tunduru, unagharimu shilingi bilioni 150.78, huku sehemu ya pili ya mradi kutoka Tunduru hadi Masasi ukigharimu shilingi bilioni 157.69.