DAWASA YAKAMILISHA MRADI WA MIALE,FURSA ZA KIUCHUMI KUONGEZEKA

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

UTEKELEZAJI wa Mradi wa Maji Miale katika Wilaya ya Mkuranga uliotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar Es Salaam (DAWASA) umekamilika kwa asilimia 100, hatua inayoashiria nafuu ya huduma ya maji kwa wakazi takribani 800 ambao hawakuwa na huduma hiyo awali katika eneo hilo.

Msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Suma Kajula ameeleza mradi ulihusisha uchimbaji na ulazaji wa mabomba yenye ukubwa wa inch mbalimbali kwa umbali wa jumla ya kilomita 1.8, kwa gharama ya Shilingi Milioni 25.

“Uekelezaji wa mradi huu unalenga kuhakikisha maji yanafika katika eneo kubwa la Miale na kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma hiyo, kwa sasa mradi umekamilika na wananchi wameanza kunufaika na tuwasihi Wananchi kujitokeza kuomba huduma ya maji Ili mradi huu ulete tija kwa kila mmoja wetu” ameeleza Mhandisi Suma.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Miale, ndugu Said Salum ameeleza kuwa mbali na kuboresha huduma ya maji, kukamilika kwa mradi huu kunaongeza fursa za kiuchumi hususani katika shughuli zote zinazotegemea uwepo wa huduma ya maji.

“Huduma bora ya maji itasaidia wananchi kutumia muda na rasilimali zao kwa ufanisi zaidi katika shughuli za uzalishaji na biashara hatua itakayochochea kukua kwa uchumi wa wananchi wa hapa Miale” ameeleza ndugu Salum.